Rais Ruto: Hatujaunda muungano na ODM

Aug 12, 2024 - 17:49
Aug 12, 2024 - 17:56
 0
Rais Ruto: Hatujaunda muungano na ODM
Rais William Ruto akiwahutubia wakazi Kaunti ya Nyamira. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Rais William Ruto ameeleza nia yake ya kushirikiana na Chama cha Orange Democratic Movement katika serikali ya Kenya Kwanza.

Akihutubia wakazi wa Kaunti ya Nyamira mnamo Jumatatu, Agosti 12, 2024, Ruto amekanusha madai ya kuunda muungano na Chama cha ODM.

Wanachama wanne kutoka ODM walijumuishwa katika serikali ya Kenya Kwanza katika Baraza la Mawaziri. 

Ruto alifafanua kuwa nia yake kuungana na ODM ni kufanya kazi pamoja kuhakikisha Wakenya wanafaidika. 

"Hatujakubaliana ya kwamba tumeunda muungano na Chama cha ODM, tumekubaliana ya kwamba tutafanya kazi pamoja, ile kazi ambayo itafaidi Wakenya wote, kwa hivyo msiwe na wasiwasi," alisema Ruto. 

Kulingana na Ruto, lengo lake kuu ni kuunganisha taifa la Kenya pamoja. 

Aliongezea kuwa kufanya kazi pamoja na ODM kutaleta manufaa mengi nchini. 

Alisema kwamba serikali ya umoja iliyoundwa itashuhudia kunawiri kwa viwango vya uchumi nchini. 

Rais aliitetea hatua yake ya kuungana na upinzani na kusema kuwa ni kwa ajili ya maendeleo ya taifa. 

"Sisi tutashirikiana. Kazi yangu ya muhimu kuhakikisha kwamba tunaunganisha Kenya iwe moja," alieleza Rais. 

Alihoji kuwa kwa kujumuisha viongozi kutoka upinzani kutapanua wiko wa maarifa kuhusu maendeleo ya taifa. 

Ruto alisema kuwa ni wakati sahihi kwa taifa kushirikiana ili kufanya maendeleo bila ya kuzingatia wala kuegemea mirengo ya kisiasa na vyama. 

Rais aliwaahidi Wakenya atafanya kila jitihada kuhakikisha wanafaidika na miradi ya serikali ya Kenya Kwanza.

Alisema kwa sasa Kenya imekuwa na umoja kwa kuwa Wakenya wameunganishwa na kuwa kitu kimoja hivyo basi kuwapa nafasi ya kutekeleza miradi ya serikali. 

"Imefika mahali ambao ni ya muhimu sio faida ya kiongozi ama sio faida ya chama, la muhimu ni faida ya Wakenya wakiwa pamoja... muhimu ni nchi yetu ya Kenya," alisema. 

Aliwapongeza viongozi na Wakenya kwa kukumbatia serikali mpya aliyoiunda baada ya kufanya marekebisho katika Baraza la Mawaziri. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow