DCI Yawakamata Washukiwa Wawili Endebess Wanaohusishwa na Wizi

Aug 29, 2024 - 18:59
 0
DCI Yawakamata Washukiwa Wawili Endebess Wanaohusishwa na Wizi
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wamewakamata washukiwa wawili wanaoaminika kuhusika na visa vya wizi wa pikipiki katika eneo la Endebess, Trans Nzoia. 

Washukiwa hao waliotambuliwa kwa jina la Sammy Mwangi Muriithi na Denis Wanjala Simiyu walinaswa wakati wa uvamizi katika gereji yao ya Ex-Japan Spares iliyoko eneo la Veterinary mjini Kitale.

Operesheni hiyo iliyofanywa na maafisa hao, ilifuatia ripoti za kijasusi zilizoonesha kuwa pikipiki zilizoibwa wakati wa uhalifu zilikuwa zikipelekwa kwenye gereji.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na DCI, pikipiki hizo zilivunjwa na kuuzwa kama vipuri kwa wanunuzi ambao hawahusiki na wizi huo.

"Taarifa za kijasusi zilifichua kuwa pikipiki kutoka kwa waathiriwa wa wizi na mauaji zilipelekwa kwenye gereji, zikasambaratishwa na kuuzwa kama vipuri kwa wanunuzi wasio na hatia," DCI ilisema. 

Gereji hiyo sasa imefungiwa kama eneo la uhalifu, huku wachunguzi wakikusanya ushahidi ambao unaweza kuwahusisha washukiwa na uhalifu huo.

Washukiwa hao wawili kwa sasa wako rumande na wanashughulikiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kukamatwa kwa watu hao kumekuja kama sehemu ya msako mkali dhidi ya magenge ya uhalifu yanayojihusisha na wizi wa kimabavu, hasa wale wanaolenga waendesha pikipiki. 

DCI imewahakikishia umma kuwa juhudi zote zinafanywa ili kusambaratisha magenge hayo na kuwafikisha waliohusika mbele ya sheria.

Wakaazi wa Endebess wameelezea kufarijika kwa kukamatwa kwa watu hao, kwani hivi karibuni mji huo umekumbwa na ongezeko la uhalifu unaohusisha wizi wa pikipiki. 

DCI wamewataka wananchi kuwa waangalifu na kuripoti shughuli zozote zinazotiliwa shaka kwa mamlaka.

Washukiwa hao wanatarajiwa kukabiliwa na mashtaka yanayohusiana na wizi, mauaji, na biashara haramu ya mali ya wizi.

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow