Makala:Ibilisi asiyemuacha binadamu kamwe

Aug 10, 2023 - 09:47
Aug 10, 2023 - 09:54
 0
Makala:Ibilisi asiyemuacha binadamu kamwe
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Kujinyonga ndio njia ya mkato inayotumika mara kwa mara na watu waliozidiwa na ugumu wa maisha ,waliokata tamaa na wenye msongo wa mawazo.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shule ya mafunzo ya Swiss Forensic kutokana na visa zaidi ya elfu sita vilivyosajiliwa,zaidi ya elfu moja ni ya watu waliojitia kitanzi kwa njia ya kujinyonga ambayo ni asilimia kumi na tisa nukta saba ya visa ya kujiuwa.

Kutokana na utafiti huo,visa hivyo vya kujinyonga havionyeshi utofauti wowote kati ya wanaume na wanawake ila utafiti huo wa Swiss Forensic umefichua kuwa wanawake wengi hujitia kitanzi kutokana na historia ya ugonjwa wa kiakili ilhali wanaume wanatumia njia hii kutokana na utambuzi wa somatiki(somatic diagnoses)inayohusiana na maumivu ya mwili,magonjwa na hali ngumu ya kimaisha.

Nchini kenya visa vya watu kujitia kitanzi vinaongezeka kila uchao.

Inaripotiwa kuwa mtu mwenye umri wa chini zaidi kujinyonga alikuwa na umri wa miaka tisa ilhali wa juu zaidi alikuwa na miaka sabini na sita. 

Wizara wa afya ilirikodi visa mia nne themanini na tatu vya watu waliojinyonga mwaka uliopita.

Leo hii tunaangazia mtazamo ya jamii ya Waluhya juu ya watu wanaojitia kitanzi kwa njia hiyo.

Wazee wenye busara katika jamii hii ndio wanaojihusisha na shughuli nzima za kufanya matambiko katika eneo la tukio.

"Unatafuta yule mzee ambaye amekuwa kiumri anaenda kukataza ile kamba aliyojinyonga nayo,"alisema James Atsangu, mmoja wa wazee wa Jamii ya Waluhya. 

Kuna baadhi ya vifaa ambavyo hutumika katika shughuli hizo za tambiko kwa ajili ya kufukuza kile wanachoamini kuwa roho mbaya ili kuzuia madhara zaidi kutoka kwa aliyejinyonga.

Mbuzi ndiyo mnyama ambaye hutumika mara nyingi kufurahisha roho ili kuacha kusumbua familia kwa mikosi. 

Mbuzi wa jinsia tofauti huchinjwa kulingana na jinsia ya aliyejinyonga,mzee wa jamii hiyo James Atsangu anaeleza zaidi.

"Mwanaume akijinyonga wanachinja mbuzi wa kiume kwa sababu ni mwanaume, wa kike kwa sababu ni mwanamke alijinyonga,"alisimulia Atsangu. 

Haja kubwa kutoka kwa mbuzi inayotambulika kwa jamii hiyo kama "busee" hutumika kusafisha na kutakasia eneo la tukio la kujinyongea ili kuzuia tukio jingine kufanyika tena.

"Hawachinji popote, wanachinja eneo ambalo amejinyongea, atatumia ile" busee" kutandaza hapo ili kuzuia tukio ingine kufanyia,"aliendelea kusimulia. 

Kama ilivyo kawaida katika jamii nyingi,Waluhya wanaamini kwamba mungu ndiye mpaji wa uhai na ndiye atakayeuchukua mwisho wa maisha.

Vile vile wanaamini mtu aliyejitia kitanzi huleta nuksi katika jamii,si tu jamii bali nuksi hiyo huandama kizazi baada ya kizazi endapo hawatafanya tambiko la kujizuia na nuksi hiyo.

"Hailetwi kwenye nyumba anabaki nje, a atengeneze wa jeneza lake nje," Atsangu alieleza. 

Baada ya kufanya tambiko hilo vifaa hivyo hutupwa maeneo ambayo hawaishi watu kama vile mtoni na msituni.

Atsangu anasimulia kuwa mtu aliyejitia kitanzi kwa kujinyonga huzikwa aghalabu wakati wa usiku.

"Hazikwi moja kwa moja kama desturi, anazikwa usiku kwenye ua la boma upande wa kushoto huo mwili hulali, inategemea alijinyongea wapi, saa ngapi,"alisema mzee huyo. 

Watu wa jamii hiyo hukaidi kuwapa watoto wao majina ya watu waliojitoa uhai ili kujikinga dhidi ya nuksi hizo kuwaandama maishani. 

Wengi waliojitia kitanzi na waliookolewa hukosa kufikiwa kwa urahisi na wataalamu wa ushauri nasaha , viongozi wa kidini na kupuuzwa na jamaa na marafiki huku wengi wao wakihisi kutengwa na jamii.

Je, ni nini sababu kuu inayochangia binadamu kufikia hatua hii ya kujitoa uhai?

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow