Gavana Lusaka afafanua swala la kuwepo kwa akaunti 352 za fedha

Jul 22, 2024 - 15:42
 0
Gavana Lusaka afafanua swala la kuwepo kwa akaunti 352 za fedha
Gavana wa Kaunti ya Bungoma Kenneth Lusaka. Picha/Hisani.

Na Robert Mutasi 

Gavana wa Kaunti ya Bungoma Kenneth Lusaka hatimaye amekuja peupe na kufafanua kwa kina uwepo wa akaunti 352 za fedha katika kaunti hiyo.

Hii inajiri baada ya vijana kutoka kaunti hiyo mnamo Julai 16, 2024, kuwasilisha maombi ya maswala kadhaa katika ofisi ya gavana ili yaangaziwe.

Akihutubia waandishi wa habari, Jumatatu, Julai 22, Lusaka alisema aliyapitia malalamishi ya vijana hao huku akiyapa baadhi ya maswala kipaumbele kama vile swala la akaunti 352 na sera ya idara ya michezo.

" Siku ya Jumanne July 16, 2024, vijana wa Bungoma waliwasilisha ombi katika ofisi yangu wakiyataja idadi kadhaa ya maswali ambayo yalihitaji uangalizi wangu," alieleza Gavana Lusaka.

Lusaka aidha alieleza kuwa vijana hao walitaka maelezo ya kina na yenye uwazi kuhusu akaunti hizo 352 za fedha za kaunti hiyo.

Lusaka alikubali kuwa gatuzi hilo linaendesha akaunti 352 katika wizara tofauti. 

" Jibu ni ndiyo. Ni ukweli kwamba Serikali ya Kaunti ya Bungoma inamiliki akaunti 352," alijibu Lusaka.

Kulingana na Lusaka, katika akaunti 352, kuna programu kama vile akaunti ya NARB, Manispaa ya Bungoma, akaunti ya Ruzuku ya Maendeleo ya Miji, akaunti za uhifadhi wa Madhumuni Maalum ya Manispaa ya Kimilili ambazo ni tisa. 

Halikadhalika alielezea kuwa kaunti hiyo inaendesha akaunti kadhaa katika Benki Kuu ya Kenya.

Kaunti hiyo pia inamiliki akaunti tatu za usimamizi wa mradi ambazo ziko katika Wizara za Maji na Utalii.

Akaunti zingine ni kama vile Akaunti za Idara ya Utawala wa Umma katika Kaunti ndoto zote tisa. 

Ziko akaunti mbili za Uendeshaji za Mabanga katika Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuendesha kilimo katika kaunti hiyo. 

“Tuna akaunti za Hospitali ya Ngazi ya Nne na Tano kwa vituo vyote vya afya katika Wizara ya Afya ambavyo ni 19. Tuna Akaunti za Makusanyo ya Mapato ya Vyanzo vyote vya kukusanya mapato ya ndani katika kaunti ambazo ni nne,” aliorodhesha Lusaka.

Serikali ya kaunti hiyo ilitenga akaunti za vituo 152 vya vyuo vya kiufundi katika Wizara ya Elimu.

“Tuna akaunti za vituo vyote vya afya na zahanati katika Wizara ya Afya ambavyo vinaleta jumla ya akaunti 352,” aliongeza Lusaka.

Spika huyo wa zamani wa seneti pia aliwahakikishia vijana hao kwamba utekelezaji wa sera za vijana na michezo uko katika hatua za mwisho. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow