Barua Kwa Raila Odinga

Na Robert Mutasi
Kwa heshima na taadhima, nachukua fursa hii adimu kukuandikia waraka huu ewe Raila Odinga, uliyekuwa waziri mkuu wa Kenya,kwa ajili kukufahamisha machache niliyo nayo.
Awali ya yote,hongera kwa kujitokeza kuwania kiti cha baraza la uanachama la Umoja wa Afrika [AUC].
Uliwakilisha taifa zima la Kenya, na endapo ungeshinda ungekuwa ushindi mkubwa kwa Kenya na Afrika nzima.
Azma yako ya kulikomboa Bara la Afrika kutoka kwenye minyororo ya mabebari na kulifanya kujitegemea kupitia kufufua uchumi na mazao yao ya ndani iko wazi.
Lakini kwa bahati mbaya hukufanikiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mnamo Jumamosi, Februari 15, 2025 Jijini Addis Ababa, Uhabeshi.
Kinyang'anyiro kilishuhudiwa katika uchaguzi huo na kuwaacha wafuasi wako roho mikononi,wengi tukiwa na matumaini kwamba utaibuka mshindi.
Karibu sana nyumbani mheshima Odinga, tunakukaribisha kwa mikono miwili pasi na kinyongo.
Ujio wako nyumbani ni wa maana sana. Jinsi unavyo fahamu hali ya kiuchumi katika taifa hili si nzuri,inayumba!
Ufisadi umekita mizizi, Idara ya Mahakama imebanwa na nguvu za dola kuu za serikali.
Odinga ombi langu kwako ni kwamba utumie fursa uliyo nayo kwa sasa serikalini ushirikiane na Rais William Ruto kufufua uchumi wa taifa hili.
Bidii na nguvu ambayo Rais alielekeza katika kampeni zako, naomba vivyo hivyo zielekezwe kwenye kulikomboa taifa na kuumaliza ufisadi.
Kwa kufanya hivyo, mtaashiaria uzalendo na mapenzi mlionayo katika taifa hili la Kenya.
Jambo jingine sa kukufahamisha ni kwamba malengo uliyokuwa nayo ya kulikomboa bara la Afrika yasifie njiani tafadhali, naomba uyafanyie kazi katika taifa hili, hivyo basi utakuwa umekomboa Kenya ndani ya Afrika.
Kwa kweli tangu uingie katika ulimwengu wa siasa, umekuwa na maono mazuri sana kwa Bara la Afrika.
Ni wakati mwafaka sasa kwako kudhihirishia taifa kwamba una uwezo wa kutekeleza maono yako kwa taifa.
Harakati zako za kupigania haki za wananchi wa kawaida tunakuomba uendeleze na utimize hapo ndipo utajizolea uaminifu kutoka kwa umma.
Rais William Ruto amekuwa nawe sako kwa bako katika kampeni zako kutoka nchi hadi nchi akikupigia debe uungwaji mkono kutoka kwa mataifa mengine.
Kama ujuavyo dawa ya deni ni kulipa, na zuri lilipwe kwa zuri, William Ruto ni kama mwanao, akilemewa msaidie kuliendesha taifa.
Jahazi likizama msaidie, njaa ikizidi msaidie alimradi kuwa naye kwa kila jambo na baadaye matunda yake tutayafurahia.
Natazamia kukuona ukifaya naye kazi pamoja na wala isiwe mwisho wa kupigania haki za wananchi, mmetoka Afrika na sasa nguvu zote ukaelekezeni kenya.
What's Your Reaction?






