Jamii ya Ogiek yalalamikia kutengwa na serikali

Aug 12, 2024 - 19:25
 0
Jamii ya Ogiek yalalamikia kutengwa na serikali
Jamii ya Ogiek. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Jamii ya Ogiek imeeneza vilio vyao kwa serikali kufuatia kutengwa na miradi ya maendeleo. 

Jamii hiyo inalalamikia kudumaa na kukwama kwa maendeleo maeneo yao kama vile barabara. 

Wakihutubia vyombo vya habari, mnamo Jumatatu, Agosti 12, 2024, katika eneo la Chepkitale, wazee wa jamii hiyo wameitaka serikali kuu na ya kaunti ya Bungoma kuwakumbuka katika miradi ya maendeleo.

Jamii ya Ogiek imepiga kambi katika maeneo ya Mlima Elgon kaunti ya Bungoma. 

Walisihi serikali kuzingatia usawa katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini bila ya ubaguzi wa kimaeneo. 

Jamii hiyo inalalamikia kutengwa na serikali ya Kaunti na ya kitaifa kwa miaka mingi sana. 

Walisema kuwa wao kama walivyo Wakenya wengine, wana haki ya kunufaika na miradi ya maendeleo kutoka kwa serikali. 

Wakazi hao wanasema suala la kutengwa na miradi ya maendeleo ya serikali limewaathiri pakubwa katika maisha yao ya kila siku. 

Ukosefu wa misaada umewafanya wakazi wengi kutaabika na kuishi maisha duni. 

Walieleza kuwepo kwa barabara mbovu katika maeneo hayo ya Chepkitale na Labot katika wadi ya Kaptama. 

Waliiomba serikali kuwakarabatia Barabara zao ili kurahisisha shughuli za usafiri maeneo hayo. 

Aidha, wakazi hao wameitaka serikali kuwafanyia maendeleo kwa kuzingatia mila na utamaduni wao. 

Walieleza kuwa kwa kuzingatia utamaduni wao wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo, watanufaika kwa kuimarisha hali zao za maisha. 

Ogiek ni mojawepo ya jamii nchini zenye idadi ndogo ya watu na zilizosalia kuzingatia na kuhifadhi kwa undani mila na desturi zao. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow