Wakazi waombwa kushirikiana na polisi kuimarisha usalama

Aug 1, 2024 - 18:38
 0
Wakazi waombwa kushirikiana na polisi kuimarisha usalama
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Idara ya usalama katika Kaunti ya Narok imewaomba wakazi katika Mji wa Narok kushirikiana na maafisa wa polisi katika operesheni ya kuimarisha usalama. 

Wakazi hao wametakiwa kupiga ripoti katika vituo vya polisi kuhusu washukiwa wa uhalifu ili kukamatwa kama njia mojawapo ya kupunguza visa vya uhalifu ambavyo vimeanza kukithiri. 

Akihutubia vyombo vya habari, mnamo Alhamisi, Agosti 1, 2024, mjini Narok, Kamishna wa Kaunti hiyo Kipkech Lotiatia amesema kuwa kwa kushirikiana na wananchi kutawezesha kutokomeza visa vya uhalifu. 

Lotiatia amesema kwamba wahalifu hao wamekuwa wakiwahaingaisha wakazi wa mji wa Narok kwa kuwaibia mali zao na kuwajeruhi. 

Kamishna huyo ameapa kuumaliza uhalifu huo chini ya muda mfupi kwa msaada wa wananchi. 

Amesisitiza kuwa watu wachache ndio wanakosesha utulivu katika mji huo wa Narok kwa kuendelea kutekeleza uhalifu. 

Aidha, ameeleza kuwa atahakikisha anawachukulia hatua kali za kisheria wahusika. 

"Naomba ushirikiano, hawa watu wawili, watatu wanatusumbua hapa, chini ya wiki moja nataka tupatane nao," alisema. 

Vile vile Kamishna huyo amewasihi wakazi hao kuwa waangalifu zaidi ili kuepukana na mitego ya wahalifu maeneo hayo. 

"Jichunge na sisi tukuchunge. Lakini kama wewe huwezi kujichunga itakuwa vigumu kwetu sisi kukuchunga," alisihi Lotiatia.

Kamanda wa Kaunti hiyo Riko Ngare, ameshukuru Kamati ya Usalama katika kaunti hiyo kwa kujizatiti kuhakikisha wanakabiliana na visa vya uhalifu. 

Amewahakikishia wakazi kuwa atafanya kazi kwa ukaribu na maafisa wa polisi kwa kufanya oparesheni ya kumaliza uhalifu. 

"Nataka nishukuru sana kamati ndogo ya usalama mjini Narok kwa kazi ambayo wanaendelea kufanya," alipongeza.

"Hiyo oparesheni iendelee kabisa mpaka tuhakikishe mambo ya usalama yamekuwa sawa sawa," aliongezea.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, kwa sasa wahalifu zaidi ya 50 wamekamatwa huku msako mkali ukiendelea. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow