Kamishna Aapa kutokomeza FGM

Aug 20, 2024 - 20:56
 0
Kamishna Aapa kutokomeza FGM
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Kamishna wa Kaunti ya Meru Jacob Ouma ameapa kukomesha visa vya ukeketaji wa wasichana katika maeneo hayo.

Kamishna alisema kuwa visa hivyo vimekithiri katika Kaunti hiyo na sasa wakati umetimia kuvitokomeza. 

Akihutubia wakazi wa Meru mnamo Jumanne, Agosti 20, 2024, Ouma alisema kuwa wasichana wengi wameharibikiwa maisha yao baada ya kukeketwa.

Kamishna alitoa onyo kali kwa wale wanaohusika kwa shughuli hizo za ukeketaji wakiwemo wanaokeketa wasichana kuwa chuma chao ki motoni.

"Nasikia wasichana wanapelekwa kukarabatiwa, Nani amekuambia Wewe unajua kutengeneza msichana kuliko Mungu?" alihoji Kamishna Ouma.

Aliwasihi machifu na naibu chifu kufanya Kila jitihada kuhakikisha wahusika wameshikwa ili kudhibit visa vya ukeketaji na kuwaokoa wasichana wanaopangwa kukeketwa. 

Aliwaamrisha machifu kufanya msako mkali ili kubaini akina mama wanaowakeketa wasichana hao ili kuchukuliwa hatua kali za kisheria. 

"Haki ya Mungu! Mimi nikipata watu wamekarabati vyombo vya watoto na kujifanya ni fundi, Nina kuhakikisha chifu wewe ndiye utakuwa wa kwanza kuumia, kwa hivyo kaa macho," alionya Kamishna. 

Ouma alihoji kuwa kuna haja ya jamii hiyo ya Meru kuenda na wakati kwa kuasi mila potofu iliyopitwa na wakati. 

Alisisitiza kuwa kitendo cha ukeketaji ni kinyume na maadili ya jamii na dini kwani inaruhusu tu watoto wa kiume pekee kupashwa tohara na wala sio vinginevyo. 

Alieleza kuwa vitendo hivyo hudhoofisha afya za watoto wa kike na hata kupelekea wengine kupoteza maisha yao.

Visa vya ukeketaji vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara kutoka maeneo tofauti nchini. 

Licha ya juhudi za serikali ya kitaifa na za kaunti kwa ushirikiano na washikadau mbalimbali na mashirika yanayohusika na haki za kibinadamu kujitahidi kukomesha bado ukeketaji umekuwa ukiendeshwa kisiri. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow