Serikali Yazidisha Vituo vya Kupimia Virusi vya Mpox

Aug 20, 2024 - 20:47
 0
Serikali Yazidisha Vituo vya Kupimia Virusi vya Mpox
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Serikali imeendeleza juhudi zake za kuweka vituo maalum haswa maeneo ya mipakani kwa ajili ya kuthibiti kusambaa kwa virusi vya nyani almaarufu Mpox.

Kituo cha hivi Karibuni kilichobuniwa ni cha Malaba One Stop Border ambacho kiko katika mpaka wa Kenya na Uganda. 

Akizungumza na waandishi wa habari mnamo Jumanne, Agosti 2024, Afisa wa Afya Kaunti ya Busia Paul Kibii alisema kuwa lengo la kituo hicho ni kuhakikisha kila mwananchi anayetoka katika taifa jirani la Uganda lazima afanyiwe vipimo vya kina ili kubaini hali yake ya afya.

Kibii alisimulia kuwa viwango vya joto mwilini ndicho kigezo muhimu wanachozingatia sana wakati wa kupima wanaopita mpakani. 

Afisa huyo alisema kuwa vipimo vya joto mwilini huchukuwa muda kubaini hali ya mtu lakini wao hufanya mara kadhaa ya vipimo hivyo ili kuhakikisha wamepata majibu ya kuridhisha. 

Kulingana na Kibii, kupanda kwa viwango vya joto mwilini huchangiwa zaidi na joto linalotokana na miale ya jua kwa hivyo huwalazimu kupima mtu na baadaye akatulia ili joto la jua lipungue na Kisha hatimaye kupimwa tena.

Endapo viwango vya joto mwilini vitazidi kuwa juu kupitia viwango vinavyostahili huwalazimu kumuweka mhusika karantini na kupiga ripoti kwa sekta ya afya ya kaunti kwa vipimo zaidi.

"Nataka niseme kwamba hii ni Malaba One Stop Border Post na hiki ndicho kituo chetu cha kufanyia vipimo ambapo watu wanaotoka Uganda wanapaswa kupita hapa, wakifika hapa lazima wapige mikono kwa sabuni vizuri," alisema. 

Alieleza kuwa serikali iko tayari kwa namna yoyote ile kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo. 

Kibii alifafanua kuwa vifaa maalum vya kufanyia vipimo ni vya kutosha kuhakikisha shughuli inasonga mbele. 

"Kwetu sisi, tumejiandaa kikamilifu, tuna vifaa vya kutosha vya kufanya mazoezi haya yote, tuna vifaa vyote vya PPE vya kutekeleza zoezi kama inavyotarajiwa," alisema.

Serikali imeweka juhudi hizi ili kuzuia kuambukizwa kwa virusi zaidi nchini. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow