St. Mathias boy Busia yatetea ubingwa wa soka kaunti ndogo ya Busia (Matayos)
Teso, Jumapili Juni 25, 2023
KNA na Absalom Namwalo
Shule ya upili ya wavulana ya St. Mathias Busia imefanikiwa kulitetea taji la soka baina ya shule za Kaunti ndogo ya Busia, ukipenda eneo bunge la Matayos, baada ya kuwavyoga mahasimu wao wakuu St. Marys Mundika Boys 2-0 kwenye fainali kali iliyochezewa uwanja wa shule ya msingi ya wavulana ya Mundika.
Magwiji hao wa mtaa wa Marachi mjini Busia walitingiza nyavu za Mundika Boys kupitia kwa mshambuliaji matata Fabian Ronny aliyefunga katika dakika ya 17 kabla ya kurejea tena dakika ya 73 na kuhakikisha wanajikatia tiketi ya kushiriki michezo hiyo kiwango cha kaunti baadaye mwezi ujao kule Nambale.
Baada ya mchuano huo, mkufunzi wa St. Mathias Boys Kevin Ojuh, amesema ni wakati sasa wa kujitayarisha kwa hatua zijazo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawakilisha Busia kwenye ngazi ya kanda ya Magharibi.
"Mnavyojua, mwaka jana tulifuzu kwa ngazi ya kanda kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, na japo hatukufanya vizuri kutokana na tajiriba finyu; mwaka huu tuko tayari kutingiza anga,"akasema mkufunzi huyo.
Naye mfungaji wa magoli yao dhidi ya Mundika Fabian Ronny ameutaja ushindi huo kama heri njema itokanayo na matayarisho mazuri na nidhamu bora.
Ikumbukwe kuwa fainali hiyo ya wavulana ilikuwa ikiwakutanisha mahasimu wawili wa soka kwa shule za upili kaunti ya Busia mara ya pili chini ya wiki moja baada awali kumenyena kwenye fainali ya Zoni ya mjini ambapo St. Mathias waliibuka na ushindi kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare muda wa kawaida.
Na kwenye soka ya akina dada, umalikia umewaendea St. Paul's Mabunge waliowanyuka St. Stephen's Lwanya Girls 2-1kupitia matuta baada ya sare tasa muda wa kawaida.
Hii ilikuwa marejeleo ya fainali ya Zoni ya Matayos juma moja lililopita ambapo Lwanya waliwapiku Mabunge.
Kwenye voliboli wasichana, Budokomi ndio bingwa baada ya kuwalima Our Lady of Mercy seti 3-1(25-21, 20-25, 25-16, 25-21).
Katika mchezo wa pete ukipenda netiboli, St. James Nasewa ndio watakaowakilisha kaunti hiyo ndogo ya Busia kwenye awamu ya kaunti.
Basketiboli wachezaji 3 kila upande itawakilishwa na Mundika Boys sawia na mchezo wa raga wachezaji 7 kila upande.
Mashindano ya kaunti ya Busia yanatarajiwa kuanza tareehe 5 mwezi ujao wa Julai kwa uandalizi wa kaunti ndogo ya Nambale.
Na ; K. N. A
What's Your Reaction?