Joho aonya wanaouza leseni za uchimbaji madini

Aug 17, 2024 - 19:32
 0
Joho aonya wanaouza leseni za uchimbaji madini
Waziri wa Madini na Uchumi wa Maziwa Hassan Joho. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Waziri wa Madini na Uchumi wa Bahari Hassan Joho ametoa onyo kali kwa wale wanaouza leseni zao za uchimbaji madini kwa waekezaji wa kigeni.

Joho alidai kuwa Wakenya wanapouza leseni hizo, wawekezaji hao hugeuka na kuanza kuwanyanyasa wachimbaji wa huku nchini. 

Akihutubia wakazi wa eneo la Kishushe, Taita Taveta, mnamo Jumamosi, Agosti 17, 2024, Joho aliwataka wahusika kukoma la sivyo sheria itachukua mkondo wake.

Wakazi wengi wamekuwa wakichukua leseni na kukawia kufanya shughuli za uchimbaji na kuanza harakati za kuzunguka huku wakiwasaka wanunuzi wa leseni zao. 

Waziri huyo alisema kuwa mienendo hiyo ya Wakenya ya kutowajibika katika kuchimba madini punde tu wanapokabidhiwa leseni kumerejesha nyuma ukuaji wa viwango vya mapato katika sekta hiyo.

"Mtu yeyote ambaye amepewa leseni akakaa nayo mwaka wa Kwanza, wa pili anazungusha kuuza hiyo leseni apate pesa, hiyo leseni lazima ifutiliwe mbali," aliamuru Joho.

Hata hivyo Joho aliwaomba Wakenya kutumia fursa hiyo kujipatia riziki ili kuimarisha hali zao za maisha. 

Uuzaji wa leseni kwa wawekezaji wa kigeni umechangia pakubwa kukithiri kwa visa vya dhuluma kwa wachimbaji wadogo eneo hilo huku wengi wao wakikadiria hasara kila kuchao. 

"Wewe kama unataka kuja kuchimba madini Kenya jipange na uwekezaji wako ukipewa leseni uingie uwanjani, lakini ukipewa leseni uzunguke nayo umuuzie huyu na yule miaka mitano inaenda tu, madini hailimwi, haichukuliwi, faida haipatikani, wananchi hawapati faida, hiyo lazima ikome," alisema. 

Joho alitilia mkazo kuwa uchimbaji madini ni njia mojawepo ambayo kama wananchi wataitumia vyema itaongeza mapato yao na kuwawezesha kujitegemea. 

Kwa mujibu wa Joho, uchimbaji haramu wa madini umekithiri katika maeneo mengi nchini na kuna haja ya kuthibiti visa hivyo. 

Wizara ya Madini iliahidi kushirikiana na Kamishna wa Kaunti ya Taita Taveta, Rhoda Onyancha kuweka mikakati ya kukabiliana na wahusika na kulinda maslahi ya wachimbaji madini wa Wakenya. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow