Kiminini Combined yatua ubingwa wa Ligi ya FKF Divisheni ya Pili Zoni ya Magharibi
Busia
Jumatatu, Agosti 7, 2023
KNA na Absalom Namwalo
Kilabu ya Soka ya Kiminini Combined kutoka kaunti ya Trans Nzoia imefuzu kushiriki ligi ya FKF Divisheni ya Kwanza msimu ujao baada ya kushinda ubingwa jumla wa Divisheni ya Pili Zoni ya Magharibi.
Kwenye fainali ya mchujo wa ligi hiyo ulioandaliwa katika uwanja wa shule ya msingi ya Otimong kaunti ya Busia, Kiminini Combined ililazimika kutumia mikwaju ya penalti na kuwaangusha mahasidi wao wakuu GFE 105 ya Eldoret 3-2 baada ya sare ya kutofungana.
Matokeo hayo yanawaacha GFE 105 wakisalia na dua la kuomba Zoo FC kuwalaza Nairobi Utd kwenye mchujo wa kufuzu ligi ya NSL ili nao pia kujikatia tiketi hiyo ya Divisheni ya Kwanza msimu kesho.
Kiminini Combined inayofadhiliwa na mbunge wa Kiminini Bwana Maurice Kakai Bissau na ambaye amehudhuria fainali hiyo kule Otimong, ilimaliza ya kwanza kwenye Zone B kabla ya kuwalima Bungoma Stars ya Zoni A' 2-0 kwenye semi fainali ya mchujo huo na hivyo kutinga fainalini.
Kakai aliwarai wanaspoti kujituma huku akitoa wito kwa shirikisho la kandanda FKF kuhakikisha viwango vya spoti vinanawiri msimu ujao.
Kwa upande wao GFE 105 waliomaliza wa pili katika Zoni B' waliwaadhibu bingwa wa Zoni A' Compel FC ya Webuye 2-0 kwenye nusu fainali ya pili ya mchujo huo wa FKF Divisheni ya Pili Magharibi ya Kenya.
Mwakilishi wa Kaunti ya Busia Compel FC ya kutoka eneo la Lukolis Teso Kusini, Opet FC, walijikwaa dakika za mwisho mwisho na kumaliza wa tatu baada ya kuongoza Zone A' mkondo wa kwanza na hata pia sehemu kubwa ya mkondo wa Pili, na hivyo watalazimika kurejelea ligi hiyo ya Divisheni ya Pili msimu ujao; japo watalazimika kuhimili upinzani mkali kutoka kwa majirani wao Malaba Giants na wageni Obuccun Border FC
Nao Kiminini Combined baada ya kufuzu wanacho kibarua kigumu cha kufanikisha ndoto ya kucheza ligi ya NSL wanapotarajia kukabiliana na wazoefu wa Green Commandoes, Bindo Utd, MOFA, Sigalagala Poly, GDC Nakuru, St Joseph's Youth Nakuru, Nyota FC, Bungoma Superstars, Sunderland Keroche miongoni mwa wengine.
Courtesy ; K. N. A
What's Your Reaction?