Kuria Kimani atetea uteuzi mawaziri kutoka chama cha ODM

Jul 30, 2024 - 18:56
Jul 30, 2024 - 21:14
 0
Kuria  Kimani atetea uteuzi mawaziri kutoka chama cha ODM
Mbunge wa Molo Kuria Kimani. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Mbunge wa Molo Francis Kuria Kimani ameunga mkono hatua ya Rais William Ruto kufuatia uteuzi wa wanachama wa Chama Cha Orange Democratic Movement katika Baraza lake la Mawaziri.

Rais aliwateua wanachama wanne katika baraza lake akiwemo aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho, John Mbadi, Opiyo Wandayi na Wycliffe Oparanya.

Akizungumza na wakazi wa eneo bunge la Molo,mnamo Jumanne, Julai 30, 2024, Kimani amesema uteuzi huo utawezesha kuunda serikali yenye umoja.

Amemsifia Rais kwa hatua hiyo akisema kuwa kujumuisha viongozi katika serikali kutoka upinzani huchochea taifa kupiga hatua katika sekta ya miradi ya maendeleo na kuleta utulivu katika mazingira ya kazi.

Amewatetea wanachama walioteuliwa kutoka mrengo wa upinzani kuwa wana haki kama Wakenya wengine kujumuishwa serikalini na kufanya kazi bila ubaguzi. 

Kimani amefafanua kuwa Kenya ni nchi ya kidemokrasia na ina katiba inayomlinda kila Mkenya bila ya kuzingatia mrengo wake wa kisiasa. 

"Kwani hawa watu wa ODM sio watu? Kenya ni yetu sisi wote," alisema Kuria Kimani.

Aidha mbunge huyo amesema kuwa uteuzi huo umeweza kuvunja minyororo ya ukabila uliokuwa umesheheni kwa miaka mingi na kuleta Wakenya pamoja. 

"Ukitaka kufanya mkutano Molo, hakuna mkutano unaweza kufanya hapa Molo ukaongea lugha moja hadi mwisho. Hapa kuna Wakalenjin, Wajaluo, Wakisii, Wakikuyu na hata hawa vijana wengi ungewaongelesha Kikuyu hawashiki kitu," alieleza.

"Kwa hivyo sisi tunataka serikali ya umoja wa Kenya yetu," aliendelea.

Kimani aliendelea kwa kueleza kuwa upinzani una haki ya kudadisi serikali ilyoko madarakani na kutaka kujua jinsi inavyofanyia Wakenya maendeleo. 

Halikadhalika amesema kuwa upinzani una haki kama Wakenya wengine ya kujiunga na serikali bila ya kushurutishwa. 

"Hawa watu wa ODM, mpaka hai wa upinzani wanalipa ushuru na wana haki ya kutaka kujua jinsi serikali inaendesha ikiwemo kuwa ndani ya hiyo serikali," Kimani alisema.

Kufuatia uteuzi huo wa mawaziri kutoka Chama cha ODM kumekuwepo na utulivu nchini na hata wengi wa wafuasi wanaoegemea mrengo wa upinzani haswa Chama cha ODM wakionekana kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow