Malala akosolewa kwa kushambulia UDA
Na Robert Mutasi
Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Alliance katika Kaunti ya Kakamega Dennis Muhanda amemsuta Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala kwa ukosoaji wake dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.
Muhanda ametaja kauli za Malala zinazoonekana kulenga serikali kuwa hazina maana.
Akihutubia waandishi wa habari Kaunti ya Kakamega, mnamo Jumatano, Julai 31, 2024, mwenyekiti huyo amesema kuwa kuna taratibu nyingi za kuwasilisha matakwa na malalamishi pasi na kusambaratisha utulivu.
Amemtaka Malala kutumia chombo sahihi kuwasilisha malalamishi pale anapohishi hajaridhishwa.
"Katibu Mkuu ana jukwaa la kuuliza hayo maswali sio kuja kuita msafara wa hadhara," alisema Muhanda.
"Kulalamika kuhusu Musalia Mudavadi ama Wetang'ula ni mambo ambayo yalipitwa na wakati," aliendelea.
Muhanda amemsihi Malala kuacha kuikosoa serikali na badala yake kuelekeza dira yake kuunganisha jamii hiyo.
Jamii ya Waluhya imeonekana kwa miaka mingi kuwa na migawanyiko mingi kufuatia wanasiasa wakiwa wameegemea katika mirengo tofauti ya kisiasa.
"Watu wanaanza kusema mluhya ni adui ya mluhya mwingine. Kwa nini mluhya ni adui ya mluhya mwingine?" aliuliza Muhanda.
Amemtaka Malala kuridhika na mgao waliopewa viongozi wa Magharibi serikalini.
"Sisi kama Kaunti ya Kakamega hatukumpigia rais kura ambazo tunaweza kusema ya kwamba tumeachwa nje," alisema.
Malala amekuwa akilalamikia kile alichokitaja kama kutengwa na kuonewa na serikali ya Kenya Kwanza kwa jamii ya Waluhya haswa katika vyeo vya uongozi.
Kauli ya Muhanda inajiri siku chache tu baada ya Malala, Gavana wa Kaunti ya TransNzoia George Natembeya pamoja na viongozi wengine kutoka ukanda wa Magharibi kuandaa mkutano wa kujadili masuala maalum na hatima ya viongozi wa jamii ya Waluhya iliwemo uongozi.
Katika mkutano huo ulioandaliwa Kakamega, viongozi wengi walionekana kutoridhishwa na uteuzi wa mawaziri katika Baraza la Mawaziri huku wakimkosoa Rais Ruto kwa uteuzi wake mpya wa mawaziri.
What's Your Reaction?