Jamii za wafugaji wahimizwa kuasi mila potovu

Jul 8, 2024 - 15:26
 0
Jamii za wafugaji wahimizwa kuasi mila potovu
Wakazi wa chepukat na Chesra walipokea mafunzo katika shule ya msingi ya Chepukat kuhusu athari ambazo ukeketaji na ndoa za mapema husababisha kwa mtoto msichana.

Kapenguria,

Jumatatu Julai, 8, 2024

KNA na Agneta Chebet

Wakazi katika Kaunti ya Pokot Magharibi wanazidi kuhimizwa kuasi mila potovu ya ukeketaji na kuwaoza wanao wasichana mapema na badala yake kuwaelimisha kwa manufaa ya baadaye.

Shirika la Kyle Gabriel Foundation kupitia mradi wa IMARIKA wameweza kuwaelimisha wakazi wa kijiji cha Chepukat na Chesra katika wadi ya Chepareria kuhusu madhara ya ukeketaji na umuhimu wa kupeleka mtoto wa kike shule.

Kulingana na Emily Laktabai,wana programu kadhaa mojawapo ikiwa kuwainua kina mama katika makundi tofauti tofauti, kutoa hamasisho katika jamii ya wafugaji kuhusu shinda ambazo mtoto wa kike anapitia wakati anapitishwa katika ukeketaji na ndoa za mapema.

“Tumekuja kuelimisha jamii ya wafugaji athari za ukeketaji pamoja na ndoa za mapema kwa mtoto wa kike,’’ Laktabai alisema.

Shirika hilo limelenga kuleta mbinu na jinsi jamii inaweza kukataa mila hizi na kuhakikisha kwamba mtoto msichana anapata nafasi sawa na yule wa kiume shuleni akisema kuwa masomo yanaleta mabadiliko makubwa katika jamii.

Aidha wamehimiza jamii kwa jumla wageukie kuwapeleka wanao shuleni ikiwa wanatamani watoto wao wapate nafasi nzuri za kazi siku za usoni.

“Tungependa kuhimiza wale ambao bado wanaendesha mila hizi potovu wageukie kuwapeleka wanao shuleni na ninaamini kupitia masomo watoto hao watafaulu,’’ Laktabai alisisitiza.

Kwa upande wake Mercy Kiyapyap mkazi katika kaunti hio amerai wazazi na vijana wajiunge katika kufanya kampeni za Kupiga vita ukeketaji na ndoa za mapema pamoja na kuwapa watoto fursa ya kwenda shuleni.

Vilevile ameomba serikali kuingilia kati katika kuwasaka wale watoto ambao wanatoka katika familia zisizojiweza ili wasikose nafasi ya kusoma kwa sababu ya umaskini.

“Tunaomba pia serikali ijitokeze katika kuwatafuta watoto ambao wanatoka familia maskini ili tuhakikishe kwamba hakuna mtoto anabaki nyumbani kwa sababu ya umaskini,” alisema kiyapyap.

Kwa upande wake Chifu, Laurence Menach alisema kuwa wamekuwa katika safari kila uchao katika kuelimisha jamii kuhusu athari za ukeketaji na ndoa za mapema.

Wenyeji vilevile wametoa shukrani zao kwa shirika hilo wakisema wanaamini kuwa mafunzo hayo yatazaa matunda.

Aidha waliomba shirika hilo kuwajengea bweni katika shule ya wasichana ya Chepukat wakiamini kuwa mikakati kama hio itasaidia pakubwa katika kuzuia ukeketaji na ndoa za mapema.

Hisani; KNA 

 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow