Ligi Kuu ya Tanzania, '"Ulaya" ndani ya Afrika Mashariki

Jul 18, 2024 - 07:46
Jul 18, 2024 - 07:48
 0
Ligi Kuu ya Tanzania, '"Ulaya" ndani ya Afrika Mashariki
Uwanja wa Benjamin Mkapa, Tanzania. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Tanzania inazidi kutawala Afrika Mashariki katika Ulimwengu wa soka.

Taifa hilo limeonekana kupiga jeki na kuyapa maswala ya michezo haswa Kandanda kipaumbele. 

Sikuambii kulea vipaji nje na ndani ya Tanzania kuhakikisha wanaziba mapengo ya wakongwe wanapostaafu soka la kulipwa na kimataifa. 

Wafadhili na washikadau katika ligi za Tanzania wana moyo wa ukarimu na juhudi za mchwa kuhakikisha huduma za michezo hazilemazwi.

Punde tu unapotia guu lako katika taifa la Tanzania na kuwadadisi mashabiki kuhusu ligi ya Tanzania bila shaka majina ya Simba na Yanga ndiyo yatasheheni vinywani mwao maana wao ndio wamebeba ufuasi mkubwa zaidi Tanzania na pia ikizingatiwa kwamba ni mahasidi wa tangu jadi.

Namna ambavyo vilabu vya Tanzania vinavyocheza kuanzia Zanzibar hadi Tanzania Bara, kwa kweli unaweza ukasema ni "ulaya ndani ya Tanzania".

Chama cha Soka Cha Tanzania TFF kwa chini ya Wizara ya Michezo na ushirikiano wa serikali, ambayo imekuwa bega kwa bega na wizara hiyo katika kutekeleza majukumu mbali mbali ya michezo, imeboresha sana miundo-mbinu.

Viwanja kama vile kile cha Benjamin Mkapa vimejengwa katika viwango wa kimataifa.

Mashabiki lukuki bin lukufu ambao hutia nakshi na uhondo katika ligi hiyo wamechangia pakubwa kuimarika kwa mchezo wa kandanda nchini humo. 

Kila ichezwapo mechi mashabikia hufurika kama siafu na kujaza viwanja kwa ajili ya kushabikia timu za pendwa na kushudia utamu na mbwembwe za wachezaji viwanjani. 

Jambo jingine linalofanya mchezo wa Kandanda wa Tanzania kunawiri sana kwa kasi Afrika Mashariki na kati ni kwamba wanapata msaada wa maana kutoka kwa serikali na viongozi wanajitolea kuwasaidia na kuwapongeza kwa kuwazawadi mara kwa mara. 

Ligi ya Tanzania inadhamiria sana kuimarika zaidi baada ya TFF pamoja na serikali kuidhinisha rasmi matumizi ya mtambo wa video (VAR) kuanzia msimu ujao.

Shughuli hiyo iliyozinduliwa kwa uwepo wa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa aliyepongezi na kuunga mkono hatua hiyo ya kutumia VAR katika ligi ya Tanzania kama kiungo muhimu kitakachoimarisha huduma viwanjani.

"Kwa VAR, ufanisi wa waamuzi wetu bila shaka utaboreshwa, hivyo kuhakikisha uamuzi wa wazi na haki," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

"Mafanikio haya yanaimarisha sifa ya taifa letu, kuhakikisha wachezaji na mashabiki wanaweza kuamini matokeo ya mechi, bila kujali kiwango cha ushindani."Aliongezea Majaliwa.

VAR imeanzishwa katika tasnia ya soka ya Tanzania kama sehemu ya juhudi za Chama cha Soka cha Tanzania (TFF) za kuboresha sana uamuzi wa mechi kwa kupunguza makosa ya kibinadamu.

Alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa VAR katika maandalizi ya Tanzania ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 pamoja na Kenya na Uganda.

Ushirikiano mzuri baina ya serikali, Wizara ya Michezo, wachezaji na mashabiki ndio unaifanya kandanda ya Tanzania kusonga mbele kwa umahiri. 

Juhudi na nguvu ambazo Tanzania imeekeza katika michezo haswa soka, zitawaletea matunda kesho. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow