Makachero wa Bungoma wamhoji ‘yesu wa Tongaren’
Bungoma, Alhamisi, May 11, 2023
KNA na Roseland Lumwamu
Hatimaye Eliud Wekesa almaarufu kama ‘yesu wa Tongaren’ amefika mbele ya afisi ya kamanda wa polisi wa Bungoma, Francis Kooli na kuhojiwa kuhusu dhehebu na mahubiri yake yenye utata.
Akizungumza afisini mwake kamanda Kooli amesema kuwa mshukiwa huyo akipatikana na hatia mkono wa sheria utachukuliwa dhidi yake.
Kwa upande wake, Wekesa amesema kuwa hana hofu yoyote kuchunguzwa na vyombo vya usalama akijitetea na kusisitiza kuwa yeye huendesha mahubiri ya ukweli yanayojikita katika neno la mungu aliye hai.
Huku akizua utani kuwa endapo atapatikana na hatia na kufunguliwa mashtaka, mawakili watakaomsaidia kuendesha kesi hiyo ni jua na mwezi.
Mhubiri huyo alitumia fursa hiyo kumsuta pasta Paul Mackenzie kwa kuwahadaa wafuasi wake.
Aliwaelekeza waabiri mabasi wakutane na yeye Tongaren ambapo atawahubiria pasi na kuwaelekeza kufunga hadi kufa.
Alisema uchunguzi wa upelelezi ufanywe na iwapo atapatikana na hatia, akabiliwe kwa mujibu wa sheria ili awe funzo kwa wengine walio na nia mbaya ya kuwaangamiza watu.
Hayo yanajiri siku chache tu baada ya mbunge wa Tongaren John Chikati kutembelea boma la yesu wa Tongaren katika wadi ya Naitiri/Kabuyefwe.
Mbunge huyo alisikitikia namna wakenya na baadhi ya wachungaji wanaomkashifu yesu wa Tongaren kama nabii wa uongo, akimtetea kuwa mahubiri yake ni ya ukweli.
Chikati alisisitiza haja ya wakenya kutoa heshima kwa eneo bunge lake bila kulichafulia jina kama eneo lililo na baadhi ya watu wenye sifa mbaya.
Aidha mbunge huyo alitoa pesa taslimu elfu ishirini kwa mtoto wa yesu wa Tongaren ambaye ni mwanafunzi katika chuo kimoja mjini Eldoret anayesomea kozi ya biashara, akiahidi kuendelea kumpa ufadhili wa karo hadi atakapohitimu.
Bwana Chikati alimtaka yesu wa Tongaren kuhakikisha kuwa anakumbatia masuala ya masomo na kuwaruhusu wanawe pamoja na watoto wa wafuasi wake kuenda shuleni.
Mwakilishi wadi ya Naitiri/Kabuyefwe, Bwana White Wafula alimrai yesu wa Tongaren kujikita katika mahubiri ya ukweli bila kujihusisha katika visa vya kuendeleza maadili potovu na itikadi kali katika jamii.
Katika siku za hivi karibuni, masuala ya dini yametawala vinywa vya Wakenya na raia wa mataifa mengine kote ulimwenguni.
Hayo ni kufuatia pasta Paul Mackenzie wa kanisa la Goodnews International na mwenzake wa kanisa la New Life Ezekiel Odero, wakitiwa mbaroni kwa madai ya kusababisha vifo vya watu baada ya kuwaelekeza katika njia isiyofaa ya ukristo.
Pasta Mackenzie alituhumiwa kuwashurutisha watoto na watu wazima kufunga hadi kufa kwamba wakifanya hivyo watapata fursa ya kukutana na Yesu Kristo.
Kwa upande wake, Pasta Ezekiel Odero anachunguzwa kubaini ikiwa ana mahusiano yoyote na mchungaji Paul Mackenzie ambaye anaandamwa na kesi ya mauaji ya halaiki Shakahola kupitia dhehebu lake potovu.
Rais William Ruto amemteua jaji Jessie Lessit kuwa mwenyekiti wa tume maalum ya kuchunguza mauaji ya halaiki wa kanisa la Goodnews International la pasta Paul Mackenzie, Kilifi.
Vile vile, Rais Ruto alibuni jopokazi litakalotoa mwelekeo kuhusu njia mwafaka ya kuweka sheria za kudhibiti shughuli za makanisa.
Jopokazi hilo linatarajiwa pia kupendekeza mbinu za kuzuia kusambaa kwa itikadi kali za dini nchini.
Na; K.N.A
What's Your Reaction?