Serikali Imeteka Nyara Sekta Ya Elimu

Feb 4, 2025 - 11:28
Feb 5, 2025 - 09:11
 0
Serikali Imeteka Nyara Sekta Ya Elimu
Picha: Kwa Hisani.

Na Robert Mutasi

Mwanadamu aliumbiwa hisia, hisia ndizo zinazoitawala roho na moyo wake katika maisha yake yote hadi siku atakapoipa dunia mkono wa marahaba.

Hisia hizo ndizo humuelekeza kufanya shughuli tofauti tofauti. Ndani ya hisia hizo ndiko kuna chembe chembe za huruma na sehemu kubwa ya utu.

Tukiwa katika harakati za kuishi na kutangamana na wanadamu wenzetu mambo mengi tu hutokea na kuathiri pakubwa maisha yetu.

Athari hizo hubadili mienendo ya mtu kabisa. Utu na hisia huungana na kuzalisha tabia za mtu chanya na hasi zinazowaathiri wenyewe na wengine.

Tamaa hujitokeza na kuanza kukua na baadaye kuipa kutu sehemu ya utu na hapo ndipo mwanadamu hukosa huruma na kuanza kufanya madhila.

Madhila yaya haya yamesawiri peupe na vongozi wetu haswa wa kisiasa.Serikali imeuza roho ya utu na kujinyakulia roho nyeusi iliyojaa kutu.

Roho inayozidi kukua kwa kasi na kuzidi kukandamiza wanyonge ambao tayari wamelemea na gharama ya maisha. Tamaa ya roho nyeusi imeelekeza kucha zake katika sekta ya elimu.

Elimu imeanza kuyumba, imegusa sekta ambayo ni udi  wa msingi wa uchumi wa taifa ambapo ndoto wa watoto wetu , matineja na vijana wetu hukuzwa na kupata ujuzi ambao huwafaidi siku zijazo.

Tamaa ikivamia moyo na roho ya mwanadamu hupoteza macho na huruma asione hata machozi yanayomdondokea. Sekta ya elimu imetekwa nyara na wakuinasua hayupo!

Ndiyo,imetekwa nyara na majitu, tena majitu yenye macho ya darubini.Macho ambayo yana uwezo wa kuangaza hata kizani.

Macho ambayo yanatazama kila senti na kile kidogo cha mwananchi wa kipato cha chini. Mfumo mpya wa ufadhili wa elimu haujakumbatiwa vyema na wazazi na walimu vyuoni kwa sababu unalimbikizia mzigo mkubwa kwa wazazi.

Hata baada ya wazazi kuzidi kulalamikia mfumo huo kwa muda mrefu na kulia hadharani kwa jinsi wanavyopambana kulipa karo shuleni, serikali imejitia hamnazo na sasa hivi imepoteza masikio kwa Wakenya, wamesalia tu na yale masikio ya kusikia milio ya vijisenti vya wananchi wanaojituma na kujitahidi kupata riziki kupitia vibarua vya kijungu-jiko.

La ajabu na mno ni kwamba wakikosolewa na wazazi ,wanaharakati na baadhi ya washikadau wa elimu wanaghadhabika sana na kuishia kuutetea mfumo huo.

Wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu ni mojawapo ya waathiriwa wakubwa. Ufadhili wa Elimu ya Juu [HELB] umekuwa ni wenye ati ati na kutiliwa shaka.

Kucheleweshwa ufadhili huo unazidi kuwaumiza wanafunzi wengi. Kuchelewa huku kumewaacha wanafunzi hao vinywa wazi na kuwaacha wahadhiri solemba.

Inasikitisha sana kuiona serikali kujifanyia mambo yao ya miradi bila ya kuwahusisha wananchi. Inasikitisha kuiona tena serikali ikijikokota kuchukua hatua za haraka za kusuluhisha mambo yaliyopinda katika sekta ya elimu.

Nia ya serikali katika sekta ya elimu si ya kutiliwa shaka tena, iko wazi.Na uwazi huo ni wa kutisha! Nia ni kuzamisha hili jahazi la elimu ambalo lilikuwa linawafaidi wengi.

Hii ina maana kuwa siku za usoni matajiri ndiyo watakaomudu karo za elimu? Je, serikali itajivunia kwa lipi? Kuyumba huku kwa kwa elimu kutasababisha kudidimia kwa maarifa katika jamii na athari zake hazitakuwa za kupendeza kamwe.

Idadi ya wasomi nchini huenda ikapungua kwa kiwango kikubwa sana endapo serikali itatanguliza tamaa na maslahi yao binafsi kabla ya yale ya Wakenya.

Mimi na akili zangu timamu nina amini kwa asilimia mia moja serikali ina uwezo wa kuimarisha sekta ya elimu bila ya kushurutishwa lakini kwa bahati mbaya tamaa ya ulafi iliyopitiliza imeitawala.

Vilevile siasa za mapema walizozianza haziwapi nafasi ya kutekeleza waliyowaahidi wapiga kura. Ni ishara tosha kwamba serikali haitambui vilio vya wanafunzi na wazazi.

Tamaa imeipa serikasli ujasiri wa kutenda madhila ya kila aina na kulitumia jicho la darubini kuwaona Wakenya kama mazumbukuku na kwa upande mwingine kuwaona kama viteka uchumi vya kuyashibisha matumbo ya viongozi serikalini.

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow