Serikali yahimizwa kuongeza miradi katika sehemu zenye mizozo

Jun 23, 2023 - 17:00
 0
Serikali yahimizwa kuongeza miradi katika sehemu zenye mizozo
Mzee Dickson Rotich alipozuru afisi za KNA mjini Kapenguria. Picha na Richard Muhambe

Kapenguria Ijumaa Juni 23, 2023

Na Richard Muhambe

Msemaji wa jamii ya Sengwer katika kaunti ya West Pokot ameitaka serikali kuweka miradi mingi ya kimaendeleo katika sehemu zinazoshuhudia visa vya uvamizi ili kuangamiza tabia hiyo.

Akizungumza na KNA, Mzee Dickson Rotich alipendekeza kuanzishwa kwa miradi ya kilimo cha unyunyiziaji maji katika maeneo ambapo jamii zinazoishi katika mipaka ya kaunti huzozania.

Rotich alisema nyingi ya mizozo hutokana na wengi wa wakaazi kukosa kazi ya kufanya kutokana na ukosefu wa maji kwa hivyo kuamua kujihusisha na visa vya wizi wa mifugo.

“Iwapo serikali itaongeza miradi ya unyunyiziaji maji katika maeneo kame bila shaka wakaazi watajihusisha na kilimo cha mimea kwa hivyo hata kusahau tofauti zao. Kwa mfano kumekuwa na amani sana tangu kupanuliwa kwa mradi wa Weiwei Irrigation Scheme,” alieleza.

Alitaja kuwa suala la mipaka kati ya kaunti ya Pokot Magharibi na Turkana linaweza kusuluhishwa kwa urahisi kupitia miradi ya kilimo ambayo itawaunganisha wakaazi.

Hali kadhalika Mzee Rotich ameihimiza serikali kuhakikisha kila mtoto katika hayo anaenda shule kwa lazima maana wale hujihusisha na ujangili wengi wao hawakuenda shule.

“Ni vigumu sana kuhubiria mtu umuhimu wa amani na kuachana na ujangili iwapo mtu huyo hakuenda shule. Mtu aliyeenda shule hutii wito wa serikali bila kulazimishwa,” alisisitiza mzee huyo.

Alisihi serikali ianzishe shule nyingi katika maeneo husika ili watoto wengi waende shule bila kusafiri mwendo mrefu.  

Rotich alisema kuwa kuna idadi kubwa ya jamii ya Sengwer ambao wanaishi katika kaunti mbalimbali zikiwemo Elgeyo Marakwet, Baringo, Uasin Gishu na Trans Nzoia kwa hivyo wana ushawishi mkubwa katika kuhakikisha utangamano katika jamii za maeneo hayo.

Na; K. N. A

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow