Wahudumu wa afya watishia kugoma
Na Robert Mutasi
Wahudumu wa Afya katika Kaunti ya Homa Bay wametishia kugoma iwapo matakwa yao hayataangaziwa.
Walisema Idara ya Afya kaunti hiyo imefumbia macho masuala muhimu ya Wahudumu hao.
Akizungumza na vyombo vya habari, mnamo Alhamisi, Agosti 8, 2024, Katibu wa Muungano wa Manesi Nchini (KNUN), Omondi Nyonje, alisema kuwa zaidi ya wahudumu 60 waliopandishwa vyeo hawajaongezewa mishahara.
Licha ya kupandishwa vyeo, Nyonje alisema kuwa baadhi ya wahudumu walipunguziwa mishahara yao.
Hali hiyo iliwapelekea wahudumu hao kulalamikia pakubwa hatua ya idara husika ya afya ya kaunti hiyo.
Muungano huo ulieleza kwamba, hatua na taratibu muhimu zilifuatwa kabla ya barua ya kupandishwa cheo kufikia Katibu wa kaunti hiyo.
Kulingana na Katibu wa KNUN, barua hiyo ilikaguliwa katika vitengo vyote vya idara husika.
"Barua hizi zilisainiwa na kutumwa na maofisa kutoka Idara ya Usimamizi wa Rasilimali na Idara ya Afya. Inakuwaje baada ya mwezi mmoja, mtu kusema barua hizi ni bandia?" aliuliza katibu wa KNUN.
Wahudumu hao walianza kulalamikia suala hilo wakitaka kujua chanzo cha kasoro hiyo.
Baadaye waliambiwa na bodi inayohusika na masuala ya afya kuwa barua hizo za kupandishwa vyeo walizopewa zilikuwa bandia.
Sasa Muungano huo umeiomba idara ya Afya na serikali ya kaunti hiyo kushughulikia suala hilo.
"Kwa mujibu wa kanuni za Tume ya Mishahara na Tume ya Utumishi wa Umma, barua hizo za kupandishwa vyeo zifanywe jinsi zilivyosoma kwa sababu zilipitia mchakato mzima, uliopitishwa na miundo yote ya serikali, Menejimenti ya Utumishi iliipitisha, bodi ikaipitisha. Sielewi kwanini walisema ni bandia baada ya hayo yote," alisisitiza.
Muungano huo umelalamikia utendakazi wa idara hiyo na kusema kuwa imewaacha na maswali mengi.
"Hilo haliwezi kutokea katika serikali yenye mwelekeo. Je, ina maana kwamba Katibu wa kaunti, mwenyekiti wa bodi na afisa mkuu wa afya hawakujua wanachofanya walipokuwa wakitoa barua hizi?" alisema.
Barua hizo za kupandishwa vyeo zilitolewa mwezi Mei, 2024.
Hata hivyo, wahudumu hao wameipa kaunti hiyo makataa ya siki 21 kufanya marekebisho katika barua hizo la sivyo wafanye mgomo.
What's Your Reaction?