Wanyakuzi wa ardhi ya misitu waonywa vikali
Na Robert Mutasi
Waziri wa Misitu, Mazingira na Tabianchi Aden Duale amewaonya wanyakuzi wa ardhi ya misitu nchini kukoma la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Duale alisema kuwa atakabiliana na wahusika kwa udi na uvumba ili kuhakikisha misitu inalindwa.
Duale aliahidi kuweka mikakati thabiti katika wizara yake ili kuhakikisha visa vya unyakuzi wa ardhi ili kubaini kwa haraka wanaohusika.
Akizungumza kwenye hafla ya upanzi wa miche katika Kaunti ya Nairobi, mnamo Alhamisi, Agosti 15, 2024, waziri alisema kuwa wizara ya Mazingira itaanzisha msako mkali kwa wahusika kuhakikisha mashamba hayo yamerejeshwa.
Duale alidokeza kwamba kuwa na hatimiliki ya mashamba ya misitu kutafutiliwa mbali umiliki wa ardhi hiyo ya serikali.
"Rasilimali hizi ni za Huduma ya Misitu ya Kenya na ikiwa kuna watu ambao wana hatimiliki au wana umiliki fulani wacha niwaambie tu, sio chini ya uangalizi wangu kama Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi," Duale alionya.
Alipinga vikali unyakuzi huo akieleza kuwa huchangia pakubwa ukataji wa miti kiholela.
Alisisitiza kuwa kila Mkenya ana haki ya kuyatunza Mazingira wala sio kuyaharibu.
"Lazima tuhifadhi spishi zote za kijani kibichi na misitu ikijumuisha Karura, City Park, na zingine zote," alisihi.
Utunzaji mazingira umetiliwa mkazo na mataifa mengi ulimwenguni kama njia mojawepo ya kupigana na janga la athari za tabianchi.
Mabadiliko ya hali ya anga yamechangiwa pakubwa na uharibifu wa mazingira kama vile ukataji miti.
Tangu Rais William Ruto ashike hatamu ya uongozi kutoka kwa Uhuru Kenyatta, amekuwa akiendesha kampeni yake ya upanzi wa miti nchini.
Kampeni hiyo inahamasisha kila mwanachi kupanda miti kila mwezi ili kutimiza malengo ya kampeni ya upanzi wa miti takribani bilioni 15 ifikapo mwaka 2032.
What's Your Reaction?