Serikali kujenga madarasa 2200 Magharibi mwa Kenya

Aug 15, 2024 - 18:34
 0
Serikali kujenga madarasa 2200 Magharibi mwa Kenya
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Serikali imeanzisha mradi wa kujenga madarasa yapatayo 2200 katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya kwa ajili ya kuwakimu wanafunzi wa gredi ya 9.

Shughuli hiyo tayari imeng'oa nanga katika Kaunti ya Kakamega siku ya Alhamisi, Agosti 15, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Shule ya msingi ya Kakamega, mnamo Agosti 15, 2024, Mkururgenzi wa Elimu eneo la Magharibi, Jared Obiere, alisema kuwa tayari serikali imeanza kujenga madarasa 12 katika shule ya msingi ya Kakamega.

"Tumekuja hapa kuzindua mradi mkubwa sana ambao unaenda kufanywa na serikali katika shule hii. Tunajenga madarasa 12 mapya ya gredi la 9," alisema.

Kwa mujibu wa Mkururgenzi Obiere, madarasa 82 yanatarajiwa kujengwa kwenye duru ya kwanza huku mengine 420 yakitarajiwa kujenga kwenye duru ya pili katika Kaunti ya Kakamega.

Alieleza kuwa ujenzi wa madarasa ya gredi ya 9 yanatarajiwa kutumika kwa mafunzo ya Mtaala wa Umilisi (CBC).

"Haya ni maandalizi ya mpito katika madarasa ya CBC. Tunafuraha kuwa serikali imetutenga katika awamu hii ya kwanza. Kaunti ya Kakamega tuna madarasa 82 halafu awamu ya 2 itakuwa na madarasa 420, kanda nzima ya Magharibi itajenga madarasa 2200 katika kaunti zote za eneo hili na tumeanza leo," Obiere alieleza.

Aidha, mkururgenzi huyo anaamini mradi huo utakamilika kwa wakati kwa sababu ameahidi kushirikiana na mwanakandarasi ili kuhakikisha shughuli hiyo haikwami.

Madarasa hayo yanatarajiwa kukamilika mwaka huu wa 2024 ili kuwapisha wanafunzi wa gredi ya 9 kutumia kuanzia mwanzoni mwa mwaka wa 2025. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow