Wazee walionusurika kuuawa wapata misaada, serikali ikitafuta suluhu la kudumu

Jul 18, 2023 - 09:35
 0
Wazee walionusurika kuuawa wapata misaada, serikali ikitafuta suluhu la kudumu
Na K. N. A

Kilifi

Jumatatu Julai 17, 2023

KNA na Jackson Msanzu

Wazee walionusurika kuuawa na familia zao kwa tuhuma za uchawi kaunti ya Kilifi wamepata misaada ya chakula na malazi huku serikali ikiwa mbioni kudhibiti visa vya mauwaji ya wazee katika gatuzi hilo.

Janga la mauwaji ya wazee Kaunti ya Kilifi linaendelea kugonga vichwa vya vyombo vya usalama huku wazee wanaokimbilia usalama wao kwenye vituo vya uokoaji wakikosa mahitaji ya kimsingi ikiwemo malazi, chakula na maji.

Kwenye ziara ya kutembelea vituo viwili vya uokoaji katika eneo la Ganze na Malindi, maafisa wa Huduma za Jamii pamoja na washikadau mbali mbali walitathmini hali halisi ya wazee hao kabla ya kuwapa chakula, magodoro na bidhaa muhimu, huku serikali ikiahidi kutafuta mbinu za kumaliza unyanyapaa na mauwaji ya wazee uliokithiri miongoni mwa familia za Kilifi. 

Akizungumza na wanahabari, msimamizi wa Huduma za Jamii Kaunti ya Kilifi Consolata Machuko alifichua kwamba tayari wameanza juhudi za kuhusisha washikadau mbali mbali ili kuwapa afueni wazee wanaonusurika kifo huku hatua za dharura zikichukuliwa ikiwemo kuwatia nguvuni washukiwa wote wanaohusika katika kuwatishia maisha na kuwaua wazee. 

“Hali ya wazee ni mbaya kwa sababu siku haiishi kabla hujasikia mzee amefukuzwa nyumbani, ametengwa, amekatwa katwa. Kuzika wale wameuawa imekuwa kila mahali katika gatuzi letu la Kilifi. Kwa hivyo wazee wetu hawako na usalama wa kutosha ndiposa sisi kama huduma za jamii tumesema kwamba hatuwezi kufanya kazi hii peke yetu,” alisema afisa huyo. 

“Tunataka kutafuta mbinu mwafaka ya kuweza kuwalinda wazee wetu. Kama kaunti ya Kilifi tungependa kuwaleta pamoja washikadau ili tuweze kuweka vichwa vyetu pamoja ili tuone tunaweza kuanzia wapi ili kuhamasisha jamii dhidi ya kuwadhulumu wazee wetu,” Machuko aliongeza. 

Aidha Machuko alisema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau katika sekta zote ili kuihamasisha jamii ya Kilifi kuhusu malezi ya wazee katika juhudi za kuangamiza dhana potovu inayowahusisha wazee na uchawi punde majanga yanapotokea kwenye familia zao. 

“Ile mbinu tunatumia ni kuleta washikadau wote pamoja ili tuweze kuwa na kauli moja tuone tunawezaje kuwasaidia. Huu ndio wakati tumeanza na tutaleta wengine wengi na tuende katika jamii tuweze kukaa na wao tuweze kujua shida iko wapi,” alisema. 

Miongoni mwa juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu, naibu mkurugenzi katika idara ya Maendelea ya Jamii Jane Ongachi alidokeza kwamba serikali iko mbioni kuunda sheria ambazo zitawalinda wazee dhidi ya aina azote za kudhuluma ikiwemo kuuawa katika jamii kote nchini. 

"Tuko katika mchakato wa kukamilisha rasimu ya muswada wa sheria kuhusu wazee ambao mwisho wa yote utakapokuwa sheria tutashughulikia ipasavyo unyanyasaji wa wazee na kuhakikisha kuwa unadhibitiwa na kukomeshwa,"Ongachi alisema. 

Vile vile Ongachi alieza kwamba kuna haja ya juhudi za pamoja kutoka kwa sekta zote ili kukabili tatizo la mauwaji ya wazee na kuongeza kuwa idara ya huduma za jamii iko tayari na imejitolea kuhakikisha wazee wanatunzwa, wanaheshimiwa na wanaishi maisha ya heshima. 

Wazee walio okolewa wakiongozwa na Gona Konde wameomba serikali na mashirika kujitokeza na kuwasaidia na chakula na matibabu ili waweze kuishi vizuri. 

Na ; K. N. A

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow