Gavana Mutai azungumzia tuhuma za ufisadi dhidi yake
Na Robert Mutasi
Gavana wa Kaunti ya Kericho Eric Mutai amejitokeza wazi kuyajibu madai ya ufisadi ambayo yameibuliwa na vijana wa kizazi kipya cha Gen Z.
Vijana hao wamemshinikiza Gavana Mutai kuweka bayana ukweli wa mambo.
Vijana hao wamepanga kuungana na vijana wengine kote nchini kufanya maandamano ya "Nanenane" siku ya Alhamisi, Agosti 8, 2024.
Akizungumza na vijana katika mkutano uliofanyika Moi Gardens, Mnamo Jumanne, Agosti 6, 2024, Mutai amelazimika kueleza kuhusu tuhuma hizo.
Vijana kutoka kaunti hiyo wanaishtumu Kericho kwa ufisadi haswa utoaji wa zabuni usiokuwa na uwazi.
Katika mkutano huo ambao ulidumu kwa takribani masaa matatu, vijana hao waliwasilisha masuala yao kwa Gavana Mutai.
"Tumekuwa na majadiliano mazuri na vijana wa Gen Z," alisema gavana.
Suala la uwajibikaji pia limepewa kipaumbele katika mazungumzo hayo.
Wamewataka viongozi walioko mamlakani katika serikali hiyo kuwajibika katika utendakazi wao.
"Huwa inasisimua kuwa na roho nzuri na akili za wanaume na wanawake ambao wanaiheshimu sana kaunti, kwa hiyo sehemu ya mjadala wameibua mgongano wa kimaslahi kuhusu michakato ya utoaji zabuni, nimewaahidi kuwa nitaangalia na kufanya ukaguzi wa kitaalamu," alisema.
Aidha, Gavana Mutai amewaahidi vijana hao kwamba atahakikisha matangazo ya kandarasi ya kaunti yanawekwa kwenye umma ili kuwafaidi vijana watakaoafiki vigezo hivyo.
Isitoshe, amewasihi vijana hao kutumia fursa hiyo kujipatia riziki punde tu serikali ya kaunti hiyo itakapotangaza.
"Ninawaahidi vile vile nitajitolea kama gavana nitaweka zabuni wazi kwa kazi zote za kaunti kufanya zabuni iliyo wazi, " alisema Mutai.
Gavana huyo ameapa kuunda jopo maalum la kuchunguza maafisa na viongozi waliohusika na ufisadi.
Gavana huyo pia ameweka ahadi ya kufanyia ukaguzi wa kina suala la utoaji zabuni.
What's Your Reaction?