‘Hatuogopi Cameroon’ na hadithi nyingine za kocha Firat
Maoni
Na Peter Ochieng
Tangu ateuliwe kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka Harambee Stars mwezi Septemba mwaka 2021, Engin Firat amekuwa kaa la moto kwenye mioyo ya mashabiki wa timu hiyo.
Rais wa Shirikisho la soka nchini (FKF) anayeondoka Nick Mwendwa, alitangaza kwamba raia huyo wa Uturuki angeiongoza Harambee Stars kwa miezi miwili, akipewa jukumu la kuisaidia timu hiyo kufuzu dimba la dunia makala ya mwaka 2022 nchini Qatar.
Ndoto ya Qatar haikutimia huku kandarasi ya awali ya miezi miwili ikigeuka miaka mitatu. Baada ya uteuzi wake, kocha Firat alisifia taifa la Kenya, akiahidi mengi ila mwisho wa siku, yaliyoafikiwa kufikia sasa ni finyu mno.
"Huu ni mradi wa kuvutia, na nafurahi kuwa hapa. Natumai tutafaulu. Kenya ni taifa zuri kwenye soka na nipo tayari kufanya kazi hapa,” alitamka kocha huyo.
Tangu mwaka 2021, Firat ameoingoza Harambee Stars kwenye mechi 23, zaidi ya nusu zikiwa za kuwania kufuzu dimba la dunia, kipute cha taifa bingwa barani Afrika (AFCON) au mtanange wa wachezaji wanaoshiriki ligi za bara Afrika (CHAN).
Katika safari hiyo, Firat ameiongoza Stars kwenye ushindi mara tatu pekee – sawa na ushindi mara moja kila mwaka, hali inayodhibitisha mashaka waliokuwa nayo mashabiki wakati alipoteuliwa.
Kumbuka kwamba kabla ya kutua Nairobi, Firat alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Moldova, taifa lisilotambulika katika ramani ya kandanda duniani.
Waswahili wanasema kwamba mgala muue na haki yake umpe. Shirikisho la soka nchini FKF pamoja na serikali ya Kenya, wadau wakubwa kwenye soka nchini wameshtumiwa mara si moja kwa kutomlipa kocha Firat.
Si ng’ombe pia anahitaji kulishwa vyema mchana kutwaa ndiposa akamuuliwe jioni? Vipi FKF iwekeze matumiani makubwa kwa Firat ilihali halipwi?
Mwezi Septemba mwaka 2023, miaka miwili baada ya kuteuliwa kuinoa makali Harambee Stars, raia huyo wa Uturuki alilalama kuhusu kutolipwa mshahara.
“Hakuna mtu anayejitolea kwenye kandanda ya Kenya kuniliko. La kuvunja moya ni kwamba hakuna malipo ninayopata,” akanung’unika kocha huyo. Kilio chake kilimfikia Ababu Namwamba, waziri wa michezo wakati huo aliyekiri kuwa kocha Firat hakuwa amelipwa kwa mda mrefu.
“Ningependa kuwahakikishia wakenya kwamba juhudi zinawekwa ili kuona kwamba kocha wa Harambee Stars na naibu wake wanalipwa haraka iwezekanavyo,” akaahidi mbunge huyo wa zamani wa Budalang’i.
Hata hivyo, ilisalia ahadi tu! Wakati michuano ya kuwania kufuzu dimba la AFCON mwaka 2025 nchini Morocco ikiwa imeshika kasi kati ya Septemba na Novemba mwaka huu, kocha Firat alirejelea kilio chake cha kutolipwa.
Swali ambalo mashabiki wamekuwa wakijiuliza kwa mda mrefu ni kuhusu kutojiuzulu kwa kocha huyo, licha ya kutolipwa mshahara. Baadhi ya wakenya wamedai kuwa Firat huingiza ‘pesa ndefu’ kupitia kazi yake nyingine ya ‘ajenti wa wachezaji,’ ambapo wakati mmoja alishtumiwa kwa kuwashawishi baadhi ya wachezaji humu nchini kujiunga na vilabu mbali mbali duniani.
Wengi wakapigwa na butwaa, swali likiwa iweje kocha wa timu ya taifa awe ajenti au wakala? Aidha, Firat ameshtumiwa kwa kuja Kenya kutalii, hili likijitokeza mara nyingi kwamba baada ya baadhi ya mechi nje ya nchi, amekuwa akifunga safari kurejea makwao na kujitokeza wakati mechi nyingine ikikaribia.
Kocha huyo amelalamikia kuwepo kwa viwanja duni humu nchini, ukosefu wa uungwaji mkono wa mashabiki na hatua ya mechi za nyumbani za Harambee Stars kuandaliwa katika taifa jirani la Uganda, kutokana na ukarabati unaondelea kwenye nyuga za kitaifa za Nyayo na Karasani jijini Nairobi.
Baada ya Stars kuichabanga Namibia mabao 2-1 kwenye mechi ya kundi J kuwania kufuzu AFCON 2025 mwezi Septemba, kocha huyo alisema kuwa Harambee Stars haigopi Cameroon.
“Cameroon wanafaa kuanza kufikiria kuhusu jinsi ya kutushinda. Hatuogopi Cameroon,” alisema Firat.
Wakati huo, Cameroon ilikuwa ikikabiliwa na mzozo wa ndani kwa ndani baina ya serikali na shirikisho la soka chini humo. Tunaweza kusema kwamba Cameroon ilikuwa imenyeshewa wakati huo.
Harambee Stars ilinyukwa magoli 4 kwa 1, kutimiza msemo kwamba “usione simba kanyeshewa ukadhani ni paka.” Katika mechi ya mkondo wa pili, watoto wa nyumbani walishindwa goli moja kwa nunge, kabla ya kutoka sare dhidi ya Zimbabwe, matokeo yaliyozika matumaini ya Kenya kushiriki AFCON mwaka 2025.
Mechi ya mwisho dhidi ya Namibia haikuwa na umuhimu, kando na kuhitimisha ratiba, ila Kenya ilijikokota na kuokota sare ya kutofungana ugenini.
Baada ya dau la Kenya kuzama, kocha Firat alisema kuwa hata akifutwa kazi hakuna linaloweza kubadilika kwenye mpira wa Kenya. Kama ningekuwa yeye, ningejiuzulu.
Ni mwamko mpya kwamba Hussein Mohamed na Macdonald Mariga ndio rais na naibu rais wa FKF mtawalia. Kenya, pamoja na Uganda na Tazania zitaanda kipute cha AFCON mwaka 2027.
Jukumu la kwanza la Mohamed na Mariga wanapoingia afisini ni kumpiga kalamu kocha Firat. Tunahitaji mwanzo mpya tunapojiandaa kwa AFCON 2027.
What's Your Reaction?