Kalonzo Musyoka atangaza kuwania urais 2027
Na Robert Mutasi
Kiongozi wa chama cha Wiper ambaye pia ni mkuu wa Azimio la Umoja One Kenya, Kalonzo Musyoka, ametangaza nia yake ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kalonzo ameapa kupambana na Rais William Ruto kwenye kinyang'anyiro cha urais.
Kalonzo alikariri kujitolea kwake kusalia upinzani, akisisitiza kuwa dhamiri yake haitamruhusu kujiunga na serikali.
“Dhamiri yangu haitaniruhusu. Kwa upendo wa taifa hili, tutasimama kidete. Hata William Ruto anajua kuwa Kalonzo atakuwa mpinzani wake; anajua hili waziwazi,” Kalonzo alisema.
Viongozi walioandamana na kiongozi wa wiper akiwemo Jeremiah Kioni na Eugene Wamalwa walimtangaza Kalonzo kuwa kiongozi wao wakisema wamemwachilia kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuwania Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
"Tumemwachilia Raila kugombea Uenyekiti wa Tume ya AU, lakini tutaendelea kufanya kazi na Kalonzo Musyoka katika upinzani ili kudhibiti serikali," Wamalwa alisema.
Msimamo thabiti wa Kalonzo unajiri baada ya Rais Ruto kuunda upya Baraza la Mawaziri na kujumuisha wanachama wanne kutoka chama cha ODM.
Raila hata hivyo ameshikilia kuwa hakuna chama cha ODM ambacho kimeingia katika mkataba wa muungano na chama cha Ruto cha UDA.
“Si Chama cha ODM wala Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party ambayo imeingia katika makubaliano yoyote ya muungano na chama cha UDA cha Rais Ruto. Tulitarajia kubuniwa kwa masharti ya wazi ya ushirikiano kulingana na masuala tuliyoibua katika jumuia zetu mbalimbali,” Raila alisema.
Wateule wanne wa ODM ni pamoja na Mbunge na Mwenyekiti wa ODM John Mbadi (Hazina), Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Ushirika), na Opiyo Wandayi (Kawi).
What's Your Reaction?