Naibu Gavana Uasin Gishu ajiuzulu

Aug 19, 2024 - 18:34
 0
Naibu Gavana Uasin Gishu ajiuzulu
Picha:Hisani.

Na Robert Mutasi 

Naibu gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu John Barorot amejiuzulu mnamo Jumatatu, Agosti 19, 2024 kutoka wadhifa wake.

Taarifa hiyo ya kujiuzulu ilitangazwa na Gavana wa Kaunti hiyo Jonathan Bii Chelilim kupitia vyombo vya habari katika jiji la Eldoret. 

Kwa mujibu wa Chelilim, Barorot ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji katika Shirika la Kimataifa katika sekta ya Teknolojia, Mawasiliano na Habari.

Licha ya kutoa sababu ya kujiuzulu kwake Barorot, Gavana Bii hakueleza bayana jina la shirika hilo na taifa mahususi lilipo shirika hilo.

Gavana huyo aliendelea kueleza kuwa Naibu wake ataondoka ofisini mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti, 2024.

"Leo tunatangaza kujiuzulu kwa Naibu Gavana wetu Eng John Barorot ambaye amepata nafasi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa katika sekta ya ICT siku yake ya mwisho ya kazi inaweza kuwa tarehe 31 Agosti 2024." Alisema.

Bii alisema kuwa Mhandisi Barorot aliyafanya maamuzi hayo kufuatia matamanio yake ya kutaka kufanya kazi yake nje ya mazingira ya kisiasa.

Gavana alimsifia Barorot kama mchapakazi mwenye weledi wa haiba ya juu. 

"Ijapokuwa ilikuwa ni matakwa yetu kuendelea kufanya kazi pamoja na kutumia utajiri wa maarifa na uzoefu wa Mhandisi Barorot, lakini ni uamuzi wake kutafuta maslahi nje ya mazingira ya kisiasa na utumishi wa umma," aliongeza Chelilim.

Aidha, alimtaja naibu wake kama rafiki wa karibu sana ambaye wamekuwa na muamala mzuri naye tangia ashike hatamu ya uongozi wa kaunti hiyo. 

Chelilim aliwaahidi wakazi wa eneo hilo kuendelea kutekeleza miradi aliyokuwa akifanya pamoja na Barorot. 

Gavana Chelilim alitangaza kumteua naibu gavana atakayechukua mikoba yake Barorot punde tu atakapoondoka afisini mnamo September 1, 2024.

Barorot aliwapongeza viongozi na wakazi wa Kaunti hiyo kwa kuwa na imani naye katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo. 

"Ningependa kuchukua fursa hii kumshukuru Dkt Jonathan Bii kwa kunipa fursa hii ya kufanya kazi nanyi kuwatumikia wananchi wa Uasin Gishu. Nawashukuru wananchi wa Uasingishu kwa kumchagua gavana na mimi kuwa naibu katika uchaguzi Mkuu uliopita, tulikuwa na mafanikio zaidi na changamoto katika miaka miwili ," alisema Barorot.

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow