Okiya Omtata akosoa mfumo mpya wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu

Jul 20, 2024 - 16:18
 0
Okiya Omtata akosoa mfumo mpya wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu
Seneta wa Busia na Mwanaharakati Okiya Omtata. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Seneta wa Kaunti ya Busia Okiya Omtata amelalamikia kuhusu madhara ya mfumo mpya wa kufadhili vyuo, vyuo vikuu na Taasisi za Kiufundi.

Mfumo huo ulizinduliwa na serikali ya Rais William Ruto chini ya Wizara ya Elimu. 

Kulingana na Omtata, mfumo huo umewalimbikizia wazazi mizigo ya elimu ambao kwa sasa wanapambana na ya hali ya maisha. 

Seneta huyo alifichua kwamba amepokea jumbe kutoka kwa wanafunzi ambao wanawazia kuacha shule na wengine kusitisha masomo yao kutokana gharama ghali ya masomo ikiwemo karo. 

"Idadi ya wanafunzi wamenifikia wakinililia karo za juu za sasa ambazo vyuo vikuu vinawatoza kutokana na huduma wanazotoa kwa wanafunzi. Ni vyema elimu iwe nafuu kwa kwa kila mtu ili amudu kuipata," sehemu ya ujumbe ilisoma siku ya Jumamosi, July 20, 2024.

Mwanaharakati huyo hata hivyo amesisitiza kwamba wanafunzi wengi ambao hawajiwezi huenda wakaathirika pakubwa na mfumo huo. 

" Mtindo mpya wa ufadhili wa vyuo na vyuo vikuu haukufikiriwa vizuri, tunahitaji kurejea mtindo wa awali kwa wanafunzi wanaoendelea na wapya na hatimaye kuondoa ada ya masomo. Katiba ya Kenya, 2010 Kifungu cha 43 (f) kinamhakikishia kila mtu ana haki ya kupata elimu, " alisema Omtata.

Mfumo mpya wa kufadhili elimu ya juu ulizinduliwa na Rais William Ruto mnamo Mei 3, 2023, kwa nia ya kutatua masaibu yanayovikumba vyuo vikuu na Taasisi za Kiufundi na Anuai.

Mfumo huo ulipendekezwa ili kushughulikia usajili wa idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo na kutatua uhaba wa ufadhili. 

Aidha mfumo huo ulichukua nafasi ya Gharama ya Kitengo Tofauti (DUC) iliyotumiwa hapo awali kufadhili vyuo vikuu.

Chini ya mfumo huu mpya, vyuo vikuu na taasisi za TVET hazitapokea tena ufadhili wa vitalu kupitia kwa wanafunzi. 

Badala yake, ufadhili kwa wanagenzi utatolewa kupitia ufadhili wa masomo, mikopo na michango ya kaya. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow