Oscar Sudi amshambulia Miguna Miguna

Jul 29, 2024 - 15:56
 0
Oscar Sudi amshambulia Miguna Miguna
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amemshutumu mwanasheria mwenye utata Miguna Miguna kwa madai ya kuchochea uvamizi wa Jengo la bunge na ikulu wakati wa maandano ya vijana wa kizazi kipya almaarufu Gen Z.

Vijana hao wamekuwa wakiandamana mara kwa mara wakiishinikiza serikali kutupilia mbali mswada tata wa fedha 2024, kung'oa mamlakani viongozi wasiowajibika na kushughulikia suala la gharama ya juu ya maisha.

Katika video iliyoonekana kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Jumatatu, Julai 29, 2024, Sudi alionekana akitema cheche za matusi dhidi ya Miguna Miguna akimtaja kuwa "mpotoshaji".

Aidha, Sudi amesema hatua hiyo ya Miguna Miguna ya uchochezi inaiweka nchi katika hatari ya kuangamia kwani huenda kukazuka machafuko na ghasia ambayo ingesambaratisha amani. 

"Miguna Miguna wewe ni mtu bure kabisa," alisema Sudi.

"Baba mzima kama wewe... bado unachochea watoto wa Gen Z, watoto wetu sisi, sisi ndio baba watoto wa Gen Z, na wewe ndo baba yetu, yaani unaingia kwenye mitandao unakoroga kukoroga," aliendelea Sudi.

Mbunge huyo amesisitiza kwamba maandamano yasiyokuwa na amani husambaratisha mipango na juhudi za serikali za kuimarisha uchumi na hali ya maisha ya wakenya. 

" Mnataka nchi yetu ichomeke ama nini? Mnataka watu waangamizwe? Wewe ni baba wa umaskini. Hata hawa watoto wetu wa Gen Z sidhani kama wanataka kuwa maskini, sidhani kama wanafikiria kuwa maskini, lakini wewe unachochea," mbunge huyo alimzomea Miguna Miguna. 

Mwanasiasa huyo alionekana kwenye video alijitapa kwa kudai kuwa yeye ndiye alifanya mpango wa kumrejesha Miguna Miguna nchini huku akisema alikuwa na haki ya kurejea Kenya lakini sasa ni kinyume na alivyotarajia kutoka kwa mwanasheria huyo. 

"Unajua ile siku ni mimi nilikufungulia ukuje Kenya, na hiyo ilikuwa haki yako. Sikukuleta eti kwa sababu nilikuwa nakufanyia usamaria wema." Sudi aliongezea. 

Sudi alionekana kuunga mkono juhudi za vijana hao waliokuwa wakiandamana na kusema kuwa walikuwa wamefungua ukurasa mpya wa mageuzi na mbinu yenye amani ya kuwasilisha matakwa yao. 

Hata hivyo, Sudi aliwalaumu baadhi ya wanaharakati akimtaja Miguna kama mmoja wa waliokuwa kipaumbele kushinikiza uvamizi wa majengo ya serikali kama vile bunge na ikulu. 

Vilevile aliongezea kuwa mwanzo maandamano yalikuwa ya amani kabla ya kuchafuliwa na baadhi ya watu waliokuwa na nia mbaya. 

"Tunakubaliana haya mambo ya Gen Z, ikianza ilikuwa nzuri sana, hata mimi niliwaunga mkono kwa sababu mimi nilijua hawa vijana wameanza kujielewa na wanajua wako wapi na wanaenda wapi. 

Lakini sasa wakora akina Bonface Mwangi na Miguna Miguna wakaingilia, " alisema mbunge wa Kapseret. 

Sudi alidai kuwa taifa la Kenya ni mojawepo ya mataifa ambayo yana amani na utulivu ukilinganisha na mataifa mengine yanayoshuhudia ghasia mara kwa mara na mapinduzi. 

Mbunge huyo amewataka wakenya haswa vijana kutumia mbinu mwafaka kuwasilisha malalamishi yao pasi na kuzua rabsha pale wanapohisi viongozi wao wamekosea. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow