Sepp van der Berg ajiunga na Brentford kutoka Liverpool

Aug 22, 2024 - 23:03
Aug 23, 2024 - 20:35
 0
Sepp van der  Berg ajiunga na Brentford kutoka Liverpool
Sepp van der Berg. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Sepp van der Berg amejiunga na timu ya Brentford kwa mkataba wa kudumu kutoka Liverpool.

Sepp ametia wino kwa ada ya takriban kitita cha dola milioni 25 pamoja na nyongeza na mkataba wa miaka mitano. 

Beki huyo pia alikuwa akimezewa mate na miamba wa Bundesliga Bayer Leverkusen lakini Wananyuki wakamuwahi. 

Liverpool walimsajili Van der Berg kwa kifurushi cha dola milioni 4.4 mnamo mwaka wa 2019 kutoka Eredivisie PEC Zwolle na kucheza mara nne katika mechi kuu. 

Brentford wamekuwa wakimumezea mate Sepp kwa muda mrefu na kujenga uhusiano mzuri na Liverpool. 

Beki huyo wa Kati mwenye umri wa miaka 22, ameandikisha mkataba utaodumu muda wa miaka mitano.

Sepp vile vile alitumikia Preston ya Kaskazini kwa muda wa miezi 18.

Van Der Berg alionekana mara 33 katika mechi za Ligi ya Bundesliga akiwa kwenye mkopo katika klabu ya Mainz msimu uliopita. 

Timu nyingi zimekuwa zikimumezea mate Sepp lakini Brentford ilikuwa chaguo lake. 

Mkufunzi wa Brentford Thomas Frank amesifia usajili wa Sepp na kusema kwamba ataongeza makali ya Kikosikazi cha Wananyuki. 

"Sepp ni beki wa kati mwenye kiwango kizuri na ana uwezo wa kuimarika zaidi," alisema. 

"Anaendana na tamaduni zetu na jinsi tunavyotaka kucheza, ni mwepesi, anasoma michezo vizuri na anaundwa na mpira katika kujenga na katika hatua za ulinzi," aliongezea. 

Frank anaamini Sepp kwa umahiri wake ataendana sambamba na kikosi chake. 

"Sepp ni mhusika mzuri, na Nina hakika kwamba ataendana vyema na kundi na kutusaidia kusonga mbele," alisema Frank.

Van Der Berg amecheza mechi 35 katika mashindano yote na kufunga mabao matatu. 

Brentford tayari imemsajili mchezaji mwingine kutoka Liverpool, Fabio Carvalho katika majira ya joto kwa dili ya dola milioni 27.5. 

Carvalho pia alitumikia klabu ya Hull City kwa mkopo huku Leicester City na Southampton wakimumezea mate. 

Pia aliweza kutia saini ya miaka mitano katika klabu ya Wananyuki. 

Carvalho aliamua kutimkia Brentford kutafuta hatima yake baada ya kukisugua kwenye benchi jambo ambalo alilalamikia kwamba anakosa kujumuishwa katika mechi nyingi. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow