Vyuo vya ufundi vyaonywa dhidi ya kufundisha kozi zisizofaa
Kilifi, Jumamosi, Aprili 15, 2023
K.N.A Na Jackson Msanzu
Katibu mkuu wa idara ya Leba na Maendeleo ya Taaluma Geoffrey Kaituko ameonya vyuo vya kiufundi dhidi ya kufundisha kozi ambazo haziambatani na malengo ya kuwapa vijana ujuzi wa kujikimu kimaisha na kubuni mafunzo ya kuvutia watu ili kujinufaisha kibiashara.
Akizungumza na wanahabari katika hafla ya uangalizi wa mitihani ya kiufundi kaika chuo cha Mkwajuni mjini Kilifi, Katibu huyo aliahidi kufanya msako dhidi ya vyuo hivyo ili kuhakikisha mafunzo yote yanayoendelezwa yanawapa vijana ujuzi wa kujisaidia.
Katibu huyo alikuwa amejiunga na maafisa wa Mamlaka ya kudhibiti mafunzo ya kiufundi (NITA) katika chuo cha Mkwajuni ili kushuhudia kufanyika kwa mitihani ya kozi mbali mabli ikiwemo ujenzi, ushonaji nguo na utengenezaji wa magari.
Bwana Kaituko alikiri kwamba baadhi ya wasimamizi wa vyuo vya ufundi nchini wanaendesha shule hizo kibiashara, hali inayosababisha kubuni mafunzo ambayo hayazingatii malengo ya kuwapa vijana ujuzi wa kazi za mikono.
“Nakubali kwamba vyuo vingi vinaendeshwa kibiashara, wanatafuta pesa tu. Wanataka kupata faida. Watakushawishi kufanya kozi kwa sababu ipo na wanahitaji kupata pesa. Kama serikali tuko na vyuo ambavyo vinadhibitiwa na Wizara ya Elimu na Wizara ya Leba. Hivyo ndivyo vyuo vinavyopeana aina ya ujuzi unaohitajika,” Bw Kaituko alisema
“Ni jukumu la viongozi kuhamasisha vijana lakini sisi kama serikali tutafanya msako katika vyuo ambavyo vinapeana mafunzo ambayo hayafai kufundishwa katika vyuo vya ufundi,” Bwana Kaituko aliongeza.
Katibu huyo alieleza kuwa kazi za maofisini sasa zimekuwa hafifu kwa sababu ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaofuzu kila mwaka hivyo kuhimiza viongozi wa mashinani kuwahamasisha vijana kuona umuhimu wa kujiunga na vyuo vya kiufundi ili kupata ujuzi wa kujiajiri.
Aidha aliwahimiza wazazi kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watoto wao kukumbatia kazi za ufundi na kuacha kuwashurutisha kufanya mafunzo ambayo huwaacha maelfu ya vijana kuhangaika bila kazi ya kufanya.
“Ningependa kuwatia moyo wazazi kwa sababu wengi wao huwa kikwazo. Bado wako na dhana ya zamani. Mtoto akitaka kuwa fundi wa magari, stima na mabomba, wanawavunja moyo. Wanataka wawe mawakili na mahasibu. Hiyo ni sawa lakini hakuna kazi za kuwatosha watu wote wanaofuzu,” alisema.
Hata hivyo, tatizo la wanafunzi kukosa fedha za karo, kulipia mitihani pamoja na kununua vifaa vinavyohitajika wakati wa mafunzo lilionekana kurudisha nyuma juhudi za vijana wengi kwani wengi wao hulazimika kukatiza mafunzo yao.
Mkufunzi wa vyuo vya kiufundi kaunti ndogo ya Kilifi North Fredrick Saro alifichua kwamba zaidi ya asilimia 30 ya wanafunzi hulazimika kusitisha kozi zao kwa sababu ya kukosa pesa za kulipa ada ya mitihani.
Bwana Saro aliomba Mamlaka ya NITA kupunguza kiwango cha pesa zinazolipishwa mitihani ili vijana waweze kumudu malipo hayo.
“Tunapata changamoto kwa sababu vijana wetu wanasoma kisha baadaye wanashindwa kufanya mitihani kwa sababu ile ada ya kujiandikisha kwa mtihani bado iko juu. Ni ombi kama NITA wanaweza sikia waweze kupunguza,” Saro alisema.
“Kiwango cha mpito kwa wanafunzi kutoka usajili hadi kufanya mtihani hatujafikia asilimia 100. Na hii imeletwa na wanafunzi kusoma kwa muda mfupi na kurudi nyumbani punde pesa zinapohitajika,” Saro aliongeza.
Wanafunzi waliokuwa wakiendelea na mitihani yao wakiongozwa na James Kadenge waliambia wanahabari kuwa wamehangaika kupata pesa za mitihani na kuomba serikali iweze kuwasaidia ili waweze kuendeleza masomo yao zaidi.
Katibu Kaituko, ambaye alipokea malalamishi hayo aliahidi kuhusisha viongozi wa kaunti ya Kilifi ili kutafuta njia za kutatua tatizo hilo.
Kaunti ya Kilifi inajumla ya vyuo vya ufundi 41 ambavyo vinatarajiwa kubadilisha maisha ya vijana kupitia mafunzo yatakayowawezesha kujikimu kimaisha na kupungunguza viwango vya umaskini uliokithiri katika eneo hilo
What's Your Reaction?