Wakulima Washauriwa kuchukua mkopo
Na Robert Mutasi
Rais William Ruto ameshauri vikundi vya ushirika vya kahawa kuchukua mkopo nafuu kutoka kwa Hazina ya Fedha za Kahawa.
Akihutubia wakazi wa Murang’a mnamo Ijumaa, Agosti 9, 2024, Ruto alieleza kuwa vikundi hivyo vitakapochukua mikopo hiyo vitawakopesha wakulima.
Ruto alisema kwamba hatua hii itawarahisishia wakulima njia ya kuchukua mkopo.
Awali wakulima walilazimika kuchukua mikopo hiyo kutoka kwa benki tofauti nchini.
"Mkopo sio tu utaleta mapinduzi katika kilimo cha kahawa, lakini pia utawaepusha wakulima kutoka kwa wakopeshaji waharibifu," alisema Ruto.
Kulingana na Ruto, serikali imetenga shilingi bilioni 3 katika hazina ya Coffee Cherry Advance Revolving Fund kwa ajili ya kuwafaidi wakulima wa kahawa.
"Tunahimiza vyama vya ushirika wa kahawa kukopa mkopo wa bei nafuu kutoka kwa Hazina ya KSh3 bilioni ya Hazina ya Kahawa ili kuwakopesha wakulima badala ya kwenda kwenye soko la kibiashara," alisema.
Rais alisema kuwa mkopo huo utaimarisha sekta ya kahawa kwa kuwainua wakulima wengi.
Katika ziara yake katika Kaunti ya Murang’a, Ruto alizindua barabara Mitarakwa- Ha Paulo-Mari miongoni kwa barabara zingine.
Ruto alisema barabara hizo zitarahisisha usafirishaji wa kahawa kutoka mashambani hadi viwandani na sokoni.
"Tumezindua Barabara ya Mitarakwa-Ha Paulo-Mbari Ya Hiti-Gitiri-Kianjogu-Kahithe-Gatuya yenye urefu wa kilomita 31 ambayo itarahisisha upatikanaji wa masoko na viwanda vya bidhaa za mashambani katika Kaunti ya Mùrang'a," alisema.
Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa kipaumbele kupigania maslahi ya wakulima wa kahawa na majani chai nchini.
Katika mkutano huo, Rais Ruto aliandamana na naibu wake Gachagua, mawaziri, Gavana Irungu Kang'ata, wabunge, na wawakilishi wadi.
What's Your Reaction?