Wanawake walalamikia kukataliwa kwa Stella Soi
Na Robert Mutasi
Vikundi vya wanawake nchini vimelalamikia hatua ya Kamati ya Bunge kufutilia mbali uteuzi wa Stella Soi Lang'at.
Lang'at hapo awali aliteuliwa na Rais William Ruto kuwa Waziri wa Jinsia, Sanaa na Turathi.
Akina mama hao wameitaka Kamati ya Bunge kutoa maelezo kamili sababu ya kukataliwa kwake Lang'at.
Aidha, mama hao walimtetea Lang'at kuwa alistahili kupewa nafasi hiyo.
Walieleza kuwa Langat ni mwanamke anayeyaelewa masuala na maslahi ya wanawake.
Walimtaja Lang'at kuwa mkakamavu, mwenye bidii, na walitarajia makubwa kutoka kwake endapo kamati hiyo ingemuidhinisha.
Walimuomba Rais Ruto kumpa nafasi tena Lang'at kwani wanahisi kamati haikumtendea haki.
Baada ya Rais Ruto kuwateua mawaziri 20 katika baraza lake la mawaziri, walifika mbele ya Kamati ya Bunge kufanyiwa msasa.
Waliulizwa maswali tofauti ili kupima uweledi wao katika utendakazi.
Mawaziri wengi walionekana kutoa maono ya jinsi watakavyoimarisha Wizara zao na kushughulikia Wakenya.
Baada ya kupigiwa msasa, ripoti rasmi ya kamati hiyo ilitolewa na kutangazwa na Kiongozi wa Walio Wengi Bungeni Kimani Ichung'wah.
Kati ya mawaziri 20 waliopigiwa msasa, 19 ndio walikubaliwa na kamati hiyo huku mmoja akikataliwa.
Stellah Soi Lang'at, alikuwa ameteuliwa kuwa Waziri wa Jinsia, Sanaa na Turathi lakini aliachwa nje ya baraza la mawaziri.
Mawaziri walioidhinishwa wameanza kutekeleza majukukumu yao kama mawaziri.
Mnamo Alhamisi, Agosti 9, 2024 mawaziri hao walikula viapo na kujumuishwa rasmi katika serikali ya Kenya Kwanza.
William Ruto aliunda serikali umoja baada ya kufanya mabadiliko makubwa katika baraza la mawaziri.
Rais William Ruto aliwazawidi mawaziri magari ya kufanya shughuli zao serikalini.
What's Your Reaction?