Wamuchomba, Babu Owino watetea maandamano

Aug 16, 2024 - 18:42
 0
Wamuchomba, Babu Owino watetea maandamano
Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Baadhi ya wabunge wamejitokeza na kutetea maandamano ya vijana yanayotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba walidai kuwa serikali haijatatua masuala yaliyowasilishwa na vijana hao. 

Vijana hao walikuwa wakilalamikia matatizo ya gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na utendakazi wa utumishi wa umma. 

Maandamano ya wiki ijayo yanakusudia kushinikiza serikali ya Kenya Kwanza kuvunja bunge wakidai hawatekelezi wajibu wao inavyofaa. 

Viongozi hao waliahidi vijana kuwa watashirikiana nao katika harakati za kuleta mabadiliko katika taifa la Kenya. 

"Vijana wa Kenya wanapaswa kujua kwamba wanaungwa mkono na Wabunge kama sisi hapa. Hatutatishwa tena kwa tuhuma za kufadhili na kuchochea maandamano ya Gen Z," alisema Wamuchomba.

Waliishtumu serikali kwa kuwahangaisha baadhi ya viongozi kwa madai ya uchochezi wa maandamano miongoni mwa vijana, madai ambayo wameyapinga na kusema ni mbinu ya serikali kulemaza juhudi zao. 

Vijana hao pia wamekuwa wakishtumu serikali kwa utepetevu uliopelekea kukithiri kwa visa vingi vya ufisadi katika afisa za serikali. 

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alimkashifu Rais William Ruto kwa kushindwa kuweka mikakati kabambe ya kukabiliana na visa vya ufisadi katika serikali jinsi walivyotaka Vijana wakati wa maandamano ya awali. 

“Vijana wa Kenya wanaomba kuwaonyesha mageuzi unayopendekeza ili kukabiliana na ufisadi na uporaji wa rasilimali za serikali unaofanywa na watu ambao wako chini ya usimamizi wako wa moja kwa moja,” alisema Babu Owino.

Viongozi hao walielezea kuwa masuala yaliyowasilishwa na vijana kwa serikali yamepuuziliwa mbali jambo ambalo limechangia kuandaliwa kwa maandamano mengine. 

Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Busia Catherine Omanyo, hata hivyo alipinga kauli ya Rais Ruto ya kuungana na Chama cha ODM kama njia mojawepo ya kusuluhisha matatizo ya Wakenya akisema kuwa hilo halitaleta mabadiliko yoyote kwa taifa. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow