Gachagua awajibu viongozi wa Mlima Kenya Wanaotishia kugura UDA
Na Robert Mutasi
Naibu Rais Rigathi Gachagua amekanusha madai ya viongozi wa Mlima Kenya ya kutaka kugura serikali ya Kenya Kwanza.
Akihutubia wakazi wa Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga, mnamo Jumamosi, Agosti 10, 2024, Gachagua aliwasihi viongozi kukoma kutoa semi zitakazoleta mgawanyiko miongoni mwa Wakenya.
"Ukija kwa raia toa maneno yakuleta matumaini," alisihi Naibu Rais.
"Kama Mlima Kenya, hii ndiyo serikali yetu. Nimesikia viongozi wa Mlima Kenya wakisema hawawezi kuondoka serikalini. Je, tukiiacha serikali tuelekee wapi?" alisema Gachagua.
Gachagua aliwashtumu viongozi wanaoeneza uvumi huo wa kuondoka katika serikali ya Ruto.
"Kama mimi sijalalamika nani mwingine analalamika?" aliuliza.
Kwa mujibu wa Gachagua, viongozi kutoka Mlima Kenya wangali imara katika serikali na wanaunga mkono sera za Kenya Kwanza.
Aidha, Gachagua aliwaonya viongozi kutoka Mlima Kenya haswa wabunge kujiepusha na siasa za mwaka 2027 na badala yake kutimiza waliyowahidi Wakenya.
"Naambia wabunge kila mtu afanye kazi yake. Mimi na Rais ndio kusema, na kama hatujasema kila mtu akimye," alisema Gachagua.
Gachagua ameonekana mara kwa mara akiunga mkono mabadiliko yaliyofanywa na Rais William Ruto katika serikali ya Kenya Kwanza.
Naibu Rais alisema kuwa viongozi kutoka Mlima Kenya wamekumbatia serikali iliyoundwa na wako tayari kufanya kazi pamoja.
Ruto alifanya marekebisho makubwa katika serikali yake baada ya kuwateua baadhi ya wanachama kutoka chama cha Orange Democratic Movement katika baraza lake la Mawaziri.
Hatua hiyo ya Rais ilionekana kuungwa mkono na asilimia kubwa ya Wakenya.
Wengi walimsifia Ruto kwa kuunda serikali yenye umoja na kusema kwamba imeunganisha Wakenya wote.
What's Your Reaction?