Viongozi washinikiza kuachiliwa kwa wavuvi wanaozuiliwa Uganda
Na Robert Mutasi
Viongozi kutoka eneo bunge la Budalangi Kaunti ya Busia wameirai serikali ya kitaifa kushirikiana na serikali ya Uganda kuachilia wavuvi wa Kenya.
Wanajeshi kutoka Uganda waliwashika wavuvi zaidi ya 100 kutoka Kenya katika Ziwa Victoria.
Akizungumza na waandishi wa habari, mnamo Jumanne, Agosti 13, 2024, Mbunge wa Budalangi Rafael Wanjala alisema Wanajeshi wa Uganda wanakiuka sheria za nchi.
Wanjala alidai kuwa Wanajeshi hao huvuka mipaka hadi Kenya na kuwadhulumu wavuvi wa Kenya kwa kuwashika.
Kwa mujibu wa Wanjala, wavuvi wengi walioshikwa na Jeshi la Uganda hawakuwa na hatia.
Aliwasuta wanajeshi wa Uganda kwa kuwawekea hatia zisizo zao punde wanapowafikisha Uganda.
"Wanafika hapa wanachukua watu wetu wanawapeleka Uganda, wakishafika huko, wanasema Hawa watu walikuwa wamekuwa kuvua huko," alisema.
Mbunge huyo alisema kuwa kaunti hiyo imekuwa na uhusiano mwema na wananchi wa Uganda lakini jeshi ndilo linajaribu kuharibu uhusiano huo mzuri.
"Wanajeshi wa Uganda wanavuka hadi Kenya kushika watu wetu. Unajua wananchi wa Uganda ni wazuri sana lakini jeshi la Uganda wanafanya tu kazi kivyao bila sheria vile wanafanya huko, wanafikiria Kenya pia utafanya hivyo, Kenya tuko na sheria zetu," alisema Wanjala.
Aliwaonya Wanajeshi hao kukoma kuwashika wavuvi wa Kenya wasiokuwa na hatia la sivyo sheria itachukua mkono wake.
" Watu wetu wakishikwa huko hata sisi huku tutawaonesha pia sisi tuna uwezo wa kuwashika, " alionya Mbunge Wanjala.
Naibu Kamishna Kaunti ya Busia Paul Papa alieleza kuwa wamefanya jitihada za kuzungumzia na uongozi wa Uganda kuhusu suala la kuachiliwa kwa wavuvi wa taifa hili na kuahidi kuwa wanafuatilia kwa ukaribu.
"Kuna watu wetu walioshikwa na Waganda, tarehe 11 mwezi Julai walishika watu 17,tarehe tisa mwezi Julai walishika tena watu 21...hiyo ndiyo inaleta uhusiano ambao sio mzuri.Lakini serikali tukufu hatulali, Miki nimeongea na DC wa huko yeye pia wanaendeleza kuongea na watu wa huko," alisema.
Papa alisistiza kuwa kitendo cha wanajeshi wa Uganda kushika wavuvi wa Kenya kiholela bila hatia kitazalisha chuki baina ya mataifa hayo mwili.
Wavuvi wengi kutoka Kenya wamekuwa wakihangaishwa na kushikwa na wanajeshi wa Uganda wakati wanaendesha shughuli zao za uvuvi katika Ziwa Victoria.
What's Your Reaction?