Wakazi wa Turkana Washeherekea Uteuzi wa Beatrice Askul Moe

Jul 31, 2024 - 16:54
 0
Wakazi wa Turkana  Washeherekea Uteuzi wa Beatrice Askul Moe
Beatrice Askul Moe, waziri mteule katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Picha/hisani.

Na Robert Mutasi 

Wakazi kutoka Kaunti ya Turkana wameshehekea kwa kuonesha furaha yao kufuatia uteuzi wa Beatrice Askul Moe katika Baraza la Mawaziri.

Rais William Ruto alimteua Beatrice Askul Moe kama Waziri katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo Jumanne, Julai 30, 2024.

Wakizungumza na wanahabari mjini Lodwar, mnamo Jumatano, Julai 31, 2024, wakazi hao walisherehekea na kuonesha hisia zao kwa uteuzi huo huku wengi wao wakimpongezi Rais Ruto. 

Peter Aneman, mkazi wa Lodwar, ametoa shukrani zake kwa serikali ya Kenya Kwanza kwa kumteua Askul kuwa Waziri. 

Aneman ametilia mkazo suala la jinsia na usawa na kueleza kuwa Rais amefanya jambo la busara kumteua mwanamke katika Baraza lake la Mawaziri. 

Alisema kuwa hii ni ishara kuwa Rais ana imani na jinsia ya kike katika utendakazi wa serikali katika sekta tofauti. 

"Nashukuru kwa maana wamemteua mwanamke. Najua mwanamke ndio kila kitu. Kwa hivyo tunarudisha shukrani kubwa sana kwa kufanya jambo jema," alisema Aneman. 

"Sisi kama wakazi wa Turkana ya Kati tunashukuru sana kwa hayo ambayo umefanya. Kwa sababu yule ndiye mwanamke wa kwanza Turkana," aliongezea. 

Kufuatia hatua hiyo ya rais, Aneman amesema wao kama wakazi wa Turkana wamehusishwa katika serikali na wanajivunia kwa sababu kwa miaka mingi walikuwa wametengwa. 

"Sisi tunahisi tumekuwa Wakenya sasa kwa maana kutoka enzi ya Jomo Kenyatta hadi sasa hatujawahi kupata Waziri wa kike," alisema.

Amemtaka Askul kuwawakilisha na kuwahudumia Wakenya wote bila kuzingatia misingi ya kikabila na kimaeneo. 

Ben Kerio, mkazi wa Lodwar, amesema kuwa uaminifu wa Beatrice Askul ndio umemuwezesha kuteuliwa na Rais. 

Zaidi ya hayo, Kerio amesema kuwa nidhamu na heshimu yake Askul ni mojawepo ya vigezo vilivyompelekea kuteuliwa. 

"Nataka kukuambia Bi Beatrice Askul tunajua kuwa uongozi wako na heshima yako na wako na kuwa mwaminifu katika chama ndio umekupa nafasi," alinena Kerio. 

Kerio aliendelea kwa kuwarai viongozi wengine kufuata nyayo za Beatrice Askul endapo wanataka kufanikiwa. 

Peter Baran, pia ni mkazi wa Lodwar, amemsihi Askul kupigania maslahi ya taifa na Afrika Mashariki kama Waziri. 

Baada ya mchakato unaotarajiwa bungeni wa kuwapiga msasa mawaziri wateule, Moe atachukua nafasi ya Peninah Malonza. 

What's Your Reaction?

like

dislike

love

funny

angry

sad

wow