Viongozi warai vijana kufutilia mbali maandamano
Na Robert Mutasi
Viongozi wa kidini pamoja na vijana wa Kanisa la Sabato Kaunti ya Nakuru wamewataka vijana kufutilia mbali maandamano na badala yake kuitisha kikao cha mazungumzo.
Maandamano hayo yaliyopewa jina Nane Nane yanatarajiwa kufanyika mnamo Alhamisi, Agosti 8, 2024 kote nchini.
Akizungumza Nakuru wakati wa mkutano wa vijana mnamo Jumanne, Agosti 7, 2024, Mhubiri Joshua Njuguna amesema kuwa Kenya imeshuhudia kipindi kirefu cha amani.
Njuguna alisema maandamano yatachochea kuzorota kwa salama nchini.
Mhubiri huyo amewarai vijana kutoilaumu serikali kwa matatizo yanayoendelea na badala yake kumpa muda Rais William Ruto kutimizia ahadi zake.
Hata hivyo, alisema kuwa ni vyema vijana kukumbatia umoja na uzalendo ili kuwezesha taifa kufanya maendeleo.
"Kwa yale ambao yanaendelea katika nchi yetu ya Kenya, sisi hatumlaumu mtu yeyote ila tunashauri Kila mtu kwamba miaka 30 nyuma, Kenya haikuwa jinsi ilivyo lakini Amani ambao tumekuwa nayo imefanya tuweze kuwa na maendeleo," alisema Mhubiri Njuguna.
Mhubiri huyo aliwashauri vijana kujiepusha na maandamano ya ghasia.
Kulingana na Njuguna, Vijana wengi wamekuwa wakilipwa na watu wasiojulikana ili kufanya maandamano.
" Tusichome nchi yetu, tujitafutie tusipewe pesa ya Kandi ya kuharibu kwa sababu ya chuki," alisihi.
Vijana kutoka Kanisa hilo la SDA waliwaomba vijana kutumia njia iliyo sahihi kuomba haki zao kulingana na katiba.
Vijana hao wamefafanua kwamba mbinu hiyo ya majadiliano na viongozi itaifanya nchi kuwa imara.
Wameelezea kuwa maandamano mengi ya vijana mara nyingi yamekuwa yakihusisha visa vya uhalifu na vurugu.
Vijana wengi wamekuwa wakiandamana maeneo mengi nchini kuushtumu uongozi dhalimu wa serikali ya Kenya Kwanza.
What's Your Reaction?